• HABARI MPYA

    Friday, March 23, 2018

    LWANDAMINA: WELAYTA DITCHA SI NJIA YA MKATO YA YANGA KWENDA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mzambia, George Lwandamina amesema kwamba Welayta Ditcha si njia ya mkato kwa Yanga kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
    Yanga SC ya Tanzania itamenyana na Welayta Dicha ya Ethiopia katika mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, mechi ya kwanza ikifanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Aprili 6 na 8 na marudiano Addis Ababa kati ya Aprili 17 na 18, mwaka huu.
    Hiyo ni baada ya droo ya mechi hizo za mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi Kombe la Shirikisho iliyokwenda sambamba na upangwaji wa makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumatano wiki hii mjini Cairo, Misri.
    Katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu jana kutoka kwao, Zambia alipokwenda kwa mapumziko, Lwandamina amesema kwamba Yanga inahitaji maandalizi mazuri na muda wa kutosha wa timu kujipanga kwa mechi zote mbili ya nyumbani na ugenini, bila kuingiliwa na ratiba ya mashindano ya nyumbani.  
    George Lwandamina amesema Welayta Ditcha si njia ya mkato kwa Yanga kwenda makundi ya Kombe la Shirikisho 

    “Kwa kufikiria ni timu kutoka Ethiopia tunaweza kuitoa ni sawa, lakini tumetazama ubora wake? Ratiba yetu yote msimu ilikuwa rahisi kwa kufikiria. Tuliona tumepata mpinzani rahisi kutoka Shelisheli, kadhalika na Botswana. Lakini shughuli yake tuliiona, soka imebadilika mno. Soka si maneno tena. Haihitaji dharau na mzaha. Inataka mipango, uwekezaji na maandalizi,”amesema.
    Lwandamina amesema kwamba yeye kama kocha na wenzake katika benchi la Ufundi wana eneo lao la kufanyia kazi na kama ambavyo wamekuwa wakifanya vizuri siku zote, wataendelea hivyo – na ni wajibu wa wengine pia katika timu kutekeleza majukumu yao vizuri, wakiwemo viongozi ili kuwapa raha wanayoitarajia wapenzi na mashabiki.
    Lwandamina amekwenda nyumbani, Lusaka kwa mapumziko mafupi na anatarajiwa kurejea Jumatatu kuendelea na majukumu yake, Yanga.
    Aprili 1, Yanga watakuwa na mechi ya Robo Fainali ya Azam Sports Federation Cup (ASFC) dhidi ya Singida United mjini Singida na Aprili 7 watamenyana na Welayta Dicha ya Ethiopia.
    Welayta Dicha watakuwa wanakwenda Tanzania kwa mara ya pili mwaka huu, baada ya Februari kuja kucheza na na Zimamoto ya Zanzibar na kushinda kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Yanga SC imeangukia kwenye mchujo huo baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 2-1 iliyofungwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya sare 0-0 kwenye mchezo wa marudiano na wenyeji, Township Rollers Uwanja wa Taifa mjini Gaborone nchini Botswana.
    Welayta Dicha imefika hatua hii baada ya kuitoa Zamalek ya Misri kwa penalti 4-3 baada ya sare ya jumla ya 3-3, kila timu ikishinda 2-1 nyumbani kwake.
    Katika Raundi ya Awali ambayo Yanga SC iliitoa Saint Louis Suns United ya Shelisheli kwa jumla ya mabao 3-2, ikishinda 2-1 Dar es Salaam na sare ya 1-1 Mahe, Welayta Dicha iliitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, ikitoa sare ya 1-1 Uwanja wa Amaan, kabla ya kushinda 1-0 Erthiopia.
    Huu ni mwaka wa tatu mfululizo, Yanga inaangukia kwenye kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na mara ya nne kwa ujumla kihiostoria.
    Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2007 ilipotolewa na na El Merreikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 2-0 iliyofungwa Khartoum baada ya sare ya 0-0 Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
    Iliingia kwenye kapu hilo baada ya kutolewa na  Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mabao 3-0 iliyofungwa mjini Tunis, baada ya sare 0-0 Mwanza.
    Mwaka pekee Yanga ilifuzu hatua ya makundi Kombe la Shrikisho Afrika baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa ni 2016, ilipoitoa Sagrada Esperança ya Angola kwa jumla ya mabao 2-1, ikishinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kwenda kufungwa 1-0 Angola.
    Hiyo ilikuwa baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa jumla ya mabao 3-2, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na kwenda kufungwa 2-1 Alexandria.
    Katika hatua ya makundi, Yanga ilipangwa Kundi moja na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), MO Bejaia ya Algeria na Medeama SC ya Ghana. 
    Yanga ilishinda mechi moja tu dhidi ya MO Bejaia 1-0 na sare ya 1-1 na Medeama Dar es Salaam huku mechi nyingine zote nne ikifungwa, zikiwemo mbili za nyumbani na ugenini na TP Mazembe.
    Mwaka jana pia Yanga baada ya kutolewa na Zanaco ya Zambia kwa mabao ya ugenini, ikilazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam na 0-0 Lusaka, ikaenda kutolewa na MC Alger ya Algeria kwa jumla ya mabao 4-1 kwenye mchujo wa kuwania tiketi ya hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda 1-0 Dar es Sakaam na kufungwa 4-0 Algiers.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: LWANDAMINA: WELAYTA DITCHA SI NJIA YA MKATO YA YANGA KWENDA MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top