• HABARI MPYA

    Monday, March 26, 2018

    KIMWAGA APANIA KUFUFUA MAKALI ZAIDI AZAM FC BAADA YA KUREJEA KWA KISHINDO JUMAMOSI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    BAADA ya kufunga mabao mawili kwenye mechi yake kwanza msimu huu, winga wa Azam FC, Joseph Kimwaga, ameweka wazi kuwa atahakikisha anakuwa vizuri zaidi.
    Kimwaga aliyekuwa nje ya dimba tokea Agosti 24 mwaka jana baada ya kupata majeraha ya goti kwenye Uwanja wa Chuo cha Ualimu cha TTC cha mkoani Mtwara, wakati Azam FC ikijiandaa na mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ndanda ulioisha kwa matajiri hao kushinda bao 1-0.
    Mabao hayo mawili Kimwaga alifunga juzi wakati Azam FC ikiichapa Friends Ranger mabao 5-0 kwenye mchezo wa kirafiki, mengine yakifungwa na kiungo Salmin Hoza, mshambuliaji Mbaraka Yusuph na winga Enock Atta kwa njia ya mkwaju wa penalti.
    Joseph Kimwaga alifunga mabao mawili Jumamosi Azam FC ikiifunga Friends Rangers 5-0


    Winga huyo amesema kwamba wachezaji anaogombania nao namba wako fiti kuliko yeye hivyo atahakikisha anajiweka vizuri zaidi.
    “Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu amenijalia nimepona vizuri, pili nashukuru benchi la ufundi kwa kunipa nafasi leo (juzi) tatu nashukuru wachezaji wenzangu kwa sababu tumeshirikiana vizuri tumefanikisha timu imeshinda,” alisema.
    Akizungumzia mabao yake mawili aliyofunga, Kimwaga alisema kuwa: “Kwangu ni jambo jema kwa sababu ni kitu ambacho nilikuwa siku zote nawaza, siku mwalimu akinipa nafasi lazima nimwonyeshe.”
    Aidha kabla Kimwaga hajaumia mwaka jana, alikuwa kwenye kiwango kizuri na hivi sasa amerejea na moto jambo ambalo linaashiria dalili njema za kuendelea kufanya vizuri katika mechi nyingine zijazo atakazopewa.
    Kikosi cha Azam FC, kitarejea mazoezini leo saa 12 jioni kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mtibwa Sugar utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KIMWAGA APANIA KUFUFUA MAKALI ZAIDI AZAM FC BAADA YA KUREJEA KWA KISHINDO JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top