• HABARI MPYA

    Wednesday, March 21, 2018

    NGORONGORO YAENDELEZA UBABE MECHI ZA KIRAFIKI, YAITANDIKA NA MSUMBIJI 2-1 TAIFA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes imefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Msumbiji katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
    Shujaa wa Tanzania leo alikuwa winga wa klabu ya Yanga, Said Mussa Bakari ‘Side Ronaldo’ aliyepika bao la kwanza lililokuwa la kusawazisha kipindi cha kwanza, kabla ya kufunga bao la pili kipindi cha pili.
    Msumbiji walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 13 kwa penalti mfungaji Belarmino Manhce, kufuatia kipa wa Tanzania kumchezea rafu Martinho Alberto na refa Emmanuel Mwandembwa wa Morogoro kuamuru pigo hilo.
    Said Mussa 'Side Ronaldo' (kushoto) amepika bao la kwanza na kufunga la pili leo 
    Said Mussa akimuacha chini beki wa Msumbiji 
    Mfungaji wa bao la kwanza la Tanzania, Abdul Suleiman akimtoka Francesco Moda 
    Kiungo wa Ngorongoro Assad Juma akijaribu kupita katikati ya wachezaji wa Msumbiji 
    Kibwana Shomary wa Tanzania akimtoka Belarmino Manhce wa Msumbiji

    Tanzania ilisawazisha bao hilo kupitia kwa mshambuliaji wake, Abdul Suleiman dakika ya 35 akimalizia krosi nzuri ya Said Mussa Bakari ‘Side Ronaldo’. 
    Tanzania ilipoteza nafasi ya kupata bao dakika ya 59 baada ya shuti dhaifu la ovyo la kiungo wake, Assad Juma Ali kuokolewa na kipa Julio Matevel.
    Side Ronaldo akawainua vitini mamia ya Watanzania walioingia bure Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi hiyo kwa kufunga bao la pili dakika ya 71 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa kipa Julio Matevel kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Hans Masoud.
    Huu ni mchezo wa pili mfululizo Tanzania wanashinda baada ya Jumapili kuifunga Morocco bao 1-0 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Msumbiji nao waliifunga 1-0 Morocco. 
    Msumbiji walimaliza pungufu mchezo huo, baada ya mchezaji wake, Gracio Pestana kutolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa kumchezea rafu kiungo wa Tanzania, Assad Ali Juma dakika ya 65.
    Mechi hizi zilikuwa maalum kujiandaa na mechi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON U-20), mchezo wa kwanza Machi 31 Uwanja wa Taifa na marudiano wiki mbili baadaye mjini Kinshasa.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa: Aboutalib MsherI, Kibwana Shomary, Nickson Kibabage/Hans Masoud dk55, Ally Msengi, Dickson Job, Ally Ng’anzi, Assad Juma, Kelvin Nashon/Mohammed Mussa dk66, Paul Peter, Abdul Suleiman na Said Mussa/Israel Mwenda dk77. 
    Msumbiji: Julio Matevel, Belarmino Manhice, Leone Victor/Eduardo Michael dk46, Luis Sitoe/Thaimo Samuel dk58, Francisco Mola, Shelton Israel, Arlemano Anhambire/Jocahim Cumbe dk55, Gracio Pestana na Cyeny Catamo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NGORONGORO YAENDELEZA UBABE MECHI ZA KIRAFIKI, YAITANDIKA NA MSUMBIJI 2-1 TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top