• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 27, 2016

  TFF YAITHIBITISHA YANGA FAINALI ASFC, MAREFA WAFUNGIWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imeithibitisha Yanga SC kuingia fainali ya michuano ya shirikisho hilo, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Taarifa ya TFF jioni ya leo imesema Coastal Union imepoteza mechi ya Nusu Fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Yanga baada ya mashabiki wake kuwa chanzo cha Mwamuzi kuvunja mchezo huo uliofanyika Aprili 24, 2016 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
  Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana leo (Aprili 27, 2016) jijini Dar es Salaam kwa kuzingatia Kanuni ya 28(2) ya Kombe la Shirikisho. Wakati mechi hiyo inavunjwa, Yanga ilikuwa ikiongoza kwa mabao 2-1.
  Wachezaji wa Yanga SC wakiwa chini ya mwembe Uwanja wa Mkwakwani Jumapili

  Coastal Union pia imepigwa faini ya sh. 2,000,000 (milioni mbili) kwa kuzingatia Kanuni ya 42(26) ya Ligi Kuu kutokana na vitendo vya vurugu za washabiki wake wakati wa mechi hiyo. Pia TFF haitasita kufungiwa uwanja huo iwapo vitendo hivyo vya vurugu za washabiki havitakoma.
  Mwamuzi wa mchezo huo Abdallah Kambuzi amefungiwa mwaka mmoja wakati Mwamuzi Msaidizi namba mbili Charles Simon ameondolewa kwenye ratiba ya waamuzi. Adhabu hizo zimetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1) ya Ligi Kuu.
  Mchezaji Adeyum Ahmed wa Coastal Union anapelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa ajili ya hatua zaidi kutokana na kitendo chake cha kumpiga kichwa Mwamuzi wa Akiba baada ya kutolewa nje. Hata hivyo, Ahmed hakufanikiwa kutimiza azma hiyo baada ya Mwamuzi huyo kumkwepa.
  Yanga imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa mujibu wa Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu kutokana na kutoingia vyumbani kwenye mechi hiyo ya Kombe la Shirikisho.
  Vilevile malalamiko ya Coastal Union kutaka mechi hiyo irudiwe yametupwa baada ya Kamati ya Mashindano kubaini kuwa hayana msingi wowote.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TFF YAITHIBITISHA YANGA FAINALI ASFC, MAREFA WAFUNGIWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top