• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 28, 2016

  YANGA HAKUNA KULALA, TAYARI WAPO MWANZA KWA AJILI YA TOTO LAO JUMAMOSI

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeondoka asubuhi ya leo kwa ndege kwenda Mwanza kwa ajili ya mechi zake mbili mfululizo za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara Kanda ya Ziwa.
  Baada ya jana kuendeleza desturi ya ushindi katika ligi hiyo kwa kuifunga Mgambo JKT 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga inatarajiwa kucheza na Toto Africans Jumamosi Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Na baada ya hapo, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu, Mei 3 watakuwa Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kumenyana na wenyeji Stand United katika mchezo mwingine wa ligi hiyo.
  Baada ya mchezo huo, Yanga itarejea Dar es Salaam kwa maandalizi ya mchezo wake wa mchujo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Sagrada Esperanca ya Angola Mei 8, Uwanja wa Taifa.
  Yanga walipokuwa kwenye ndege asubuhi ya leo kwa safari ya Mwanza
  Baada ya mchezo huo, Ratiba ya Ligi Kuu inawapeleka Yanga Mbeya kumenyana na wenyeji Mbeya City Mei 10, mchezo ambao unaweza kuahirishwa pamoja na ule wa Mei 15 dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara kutokana na Yanga kuwa na mchezo wa marudiani na Esperanca Aprili 17 au 18 Angola.
  Kuna uwezekano Yanga ikacheza mechi zake tatu za mwisho za Ligi Kuu mfululizo dhidi ya Mbeya City, Ndanda na Majimaji uliopangwa kuchezwa Mei 21, Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
  Kwa ujumla Ligi Kuu itaendelea mwishoni mwa wiki, Jumamosi mbali na Toto na Yanga, African Sports watamenyana na Coastal Union katika mechi ya mahasimu wa Jiji la Tanga, Uwanja wa Mkwakwani, Mwadui FC watamenyana na Stand United katika mechi ya mahasimu wa Shinyanga Uwanja wa Mwadui Complex, Mtibwa Sugar na Mbeya City Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Prisons watakuwa wenyeji wa JKT Ruvu Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Jumapili kutakuwz na mchezo mtamu zaidi baina ya Simba SC na Azam FC Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA HAKUNA KULALA, TAYARI WAPO MWANZA KWA AJILI YA TOTO LAO JUMAMOSI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top