• HABARI MPYA

  Saturday, April 23, 2016

  HANS POPPE: SIMBA KWELI TUNATAFUTA KOCHA, LAKINI SI HUYU BASENA TENA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  MWENYEKITI wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe amesema ni kweli wanatafuta kocha wa kufanya kazi pamoja na kocha wao wa sasa, Jackson Mayanja lakini si Mganda mwenzake, Moses Basena.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE  jioni ya leo, Hans Poppe amesema kwamba uvumi unaoenezwa kwamba Simba inataka kumrejesha Basena si kweli.
  “Nadhani uvumi huu unatokana na kwamba Basena alikuwa hapa nchini na mimi nilikutana naye. Ila hatukukutana kwa sababu ya suala la kurudi kazini Simba, yalikuwa ni masuala yetu mengine binafsi,”amesema Poppe.
  Hans Poppe amesema Basena alikuja kwa masuala binafsi na si kurudi kazini Simba 

  Lakini Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) amekiri Simba SC ipo kwenye mchakato wa kutafuta kocha wa kufanya kazi na kocha wao wa sasa, Mayanja.
  “Mchakato unaendelea kwa umakini sana na ukimya wa hali ya juu, mambo yakikamilika yatawekwa hadharani,”amesema Poppe ambaye kwa sasa ni mmoja wa wafanyabiashara wakubwa wa usafirishaji nchini.
  Kumekuwa na uvumi kwenye mitandao ya kijamii kwamba Simba inamrejesha Basena na hiyo imetokana na kile kinachoaminika Mayanja ameshindwa kumudu vyumba vya kubadilishia nguo kutokana na migogoro ya mara kwa mara na wachezaji.
  Mayanja alianza kwa kutofautiana na beki Hassan Isihaka ambaye alifikia hadi kusimamishwa na uongozi baadaye akatofautiana na kiungo Abdi Banda ambaye ameamua kususa timu tangu mwezi uliopita.
  Katikati ya mwezi huu akatofautiana na Waganda wenzake, beki Juuko Murshid na mshambuliaji Hamisi Kiiza, mgogoro ambao hata hivyo ulizimwa kwa busara za uongozi.
  Simba wanaamini Mayanja ni kocha mzuri na amekuwa sahihi mara zote katika tofauti zake na wachezaji.
  Lakini tu anashindwa kuvumilia mapungufu ya asili ya wachezaji wa Kitanzania, ambayo wanawaambukiza na wageni, ndiyo maana wanamtafutia kocha wa kushirikiana naye atakayerejesha mshikamano baina ya benchi la ufundi na wachezaji.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HANS POPPE: SIMBA KWELI TUNATAFUTA KOCHA, LAKINI SI HUYU BASENA TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top