• HABARI MPYA

  Sunday, April 24, 2016

  KUFIKIRIA YANGA IMEPATA KIBONDE SHIRIKISHO NI KUJIDANGANYA

  MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga SC watamenyana na Sagrada Esperanca ya Angola kuwania kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwezi ujao.
  Mchezo wa kwanza umepangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Mei 6 na 8 wakati wa marudiano utafanyika Angola kati ya Mei 17 na 18.
  Hiyo inafuatia Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kufungwa 2-1 Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora, ikitoka kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

  Yanga ilianza vizuri ikicheza mechi zake nne za awali bila kupoteza hata moja, ikishinda tatu na kutoa sare moja.
  Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya Cercle de Joachim nchini Maurtius na 2-0 Dar es Salaam katika mchujo wa awali, kabla ya kushinda 2-1 Kigali dhidi ya APR na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Sagrada wao, walianzia kwenye Raundi ya Awali ya mchujo pia, ambako waliitoa Ajax Cape Town ya Afrika Kusini kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kufungwa 2-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani, kabla ya kuitoa LD Maputo ya Msumbiji kwa jumla ya mabao 2-1 ikishinda 1-0 nyumbani na kutoa sare ya 1-1 ugenini. Katika hatua ya 16 Bora, Sagrada waliitoa timu ya V. Club Mokanda ya Kongo kwa jumla ya mabao 4-1 ikishinda 2-1 ugenini na 2-0 nyumbani.
  Kwa rekodi hizi, hii si timu ya kubeza, ikitoka kushinda nyumbani na ugenini katika hatua ya 16 Bora, maana yake Yanga wanakutana na wapinzani wagumu.
  Hii inakuwa mara ya pili kwa Yanga kuangukia kwenye nafasi hii na kwa ujumla hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuingia kwenye mchujo huo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya michuano hiyo midogo ya klabu Afrika. 
  Mwaka 2007 Yanga ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia katika hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kabla ya kutoa sare ya 0-0 mjini Mwanza, hivyo kucheza na El Merreikh ya Sudan na kutoa sare ya 0-0 pia Mwanza kabla ya kufungwa 2-0 Khartoum na kutolewa.
  Mwaka 2011 Simba ilitolewa na DC Motema Pembe ya DRC kwa jumla ya mabao 2-1, ikifungwa 2-0 ugenini na kushinda 1-0 nyumbani katika kuwania hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa. 
  Na Simba iliangukia huko baada ya kufungwa 3-0 na Wydad Casablanca ya Morocco mjini Cairo, Misri katika mechi maalum ya mkondo mmoja.
  Hiyo ilifuatia TP Mazembe iliyoitoa Simba katika Raundi ya kwanza kwa jumla ya mabao 6-3, ikiifunga 3-1 Lubumbashi na 3-2 Dar es Salaam katika Raundi ya Kwanza na baadaye kuitoa Wydad katika Raundi ya Pili kuondolewa mashindanoni na CAF kwa kosa la kumtumia beki Janvier Besala Bokungu, aliyevunja mkataba kinyume cha taratibu na klabu ya Esperance ya Tunisia.
  Kwa kuwa Simba ndiyo waliyoikatia rufaa Mazembe baada ya kutolewa tu, CAF ikaamua timu hiyo zicheza na Wydad iliyotolewa pia na Mazembe kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.
  Tukirudi kwenye suala la Yanga, baada kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho, inaonekana kama wanajiona tayari wamekwishafuzu hatua ya makundi, wakati ukweli ni kwamba ni wanaingia kwenye kuwania hatua hiyo.
  Yanga wanaonekana kuidharau timu ya Angola na hesabu zao zimeanza kufikiria hatua ya makundi, jambo ambalo ni kosa. 
  Mashabiki wa Yanga wana hamu ya kuiona timu yao inafika mbali kwenye michuano ya Afrika ili kupunguza masimango ya watani wao wa jadi, Simba wenye rekodi nzuri zaidi kwenye michuano hiyo.
  Lakini hilo linawezekana tu iwapo Yanga wataacha kuidharau timu ya Angola ni kujiandaa vizuri kwa ajili ya mechi mbili za nyumbani na ugenini.
  Nataka vichwa vya wachezaji wa Yanga na benchi la Ufundi vijue kwamba wanakwenda kukutana na timu ngumu, ili wajiandae kwa mtihani mgumu.
  Tusiishi kwa mazoea au kukariri tu kwamba timu ngumu zipo Kaskazini mwa Afrika pekee, hapana – Siku hizi timu ngumu kwanza unaijua kwa matokeo yake ya awali.
  Unaanzaje kuidharau timu ambayo imeshinda hadi mechi za ugenini katika michuano ya Afrika tena dhidi ya timu ya Kongo?
  Ninachoweza kuwaambia Yanga, wanatakiwa kujipanga haswa ajili ya mechi mbili za mapema Mei dhidi ya Sagrada ili waitoe na kwenda hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KUFIKIRIA YANGA IMEPATA KIBONDE SHIRIKISHO NI KUJIDANGANYA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top