• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 22, 2016

  AZAM FC WAACHA NDEGE, WAPANDA NDEGE KUIFUATA MWADUI, YANGA SAFARI TANGA

  Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
  AZAM FC imerejea mjini Dar es Salaam jioni ya leo kutoka Tunisa ambako Jumanne ilifungwa mabao 3-0 na wenyeji Esperance na kutolewa katika Kombe la Shirikisho Afrika.
  Azam FC iliondoka Tunis jana mchana ikipitia Dubai, baada ya kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 na Esperance kufuatia kushinda 2-1 Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo.
  Na mara baada ya kuwasili, Azam FC itaunganisha ndege nyingine baadaye Saa 1:45 usiku kuelekea mjini Mwanza, ambako watalala kabla ya kesho asubuhi kuanza safari ya barabara kwenda Mwadui mkoani Shinyanga.
  Viungo Himid Mao (mbele) na Jean Baaptiste Mugiraneza wakiwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) leo
  Kushoto ni beki Erasto Nyoni anayeweza kucheza nafasi za kiungo pia

  Azam FC Jumapili wanatarajiwa kucheza na wenyeji Mwadui katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC).
  Nusu Fainali nyingine ya michuano hiyo itachewa Tanga Jumapili pia kati ya Yanga SC na wenyeji Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
  Yanga nayo imerejea leo kutoka Misri, ambako juzi ilifungwa 2-1 na wenyeji Al Ahly katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya awali kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Hata hivyo, Yanga sasa itamenyana na Sagrada Esperanca ya Angola kuwania kuingia kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika, mechi ya kwanza ikichezwa Dar es Salaam kati ya Mei 6 na 8 na marudiano ugenini kati ya mei 17 na 18.
  Yanga SC leo watalala katika hoteli ya Valley View, Kariakoo, Dar es Salaam na asubuhi mapema kesho watasafiri kwa basi lao kwenda Tanga.
  Kutoka kulia Salum Abubakar, Kipre Balou na Allan Wanga wakiwasili JNIA leo
  Ramadhani Singano 'Messi' mbele wakati wa kuwasili JNIA
  Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad (kushoto) akiwaongoza viongopzi wenzake baada ya kutoka JNIA
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM FC WAACHA NDEGE, WAPANDA NDEGE KUIFUATA MWADUI, YANGA SAFARI TANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top