• HABARI MPYA

  Ijumaa, Aprili 29, 2016

  FARID MUSSA: HISPANIA KUGUMU, LAKINI NAKOMAA HADI KIELEWEKE

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WINGA chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Farid Mussa Malik (pichani kushoto) amesema kwamba majaribio anayoendelea nayo katika klabu ya Deportivo Tenerife ya Ligi Daraja la Pili Hispania ni magumu, lakini atajitahidi afuzu.
  Akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE baada ya mazoezi ya leo, Farid amesema kwamba kinachoendela kwa sasa ni kubadilishwa kiuchezaji baada ya benchi la Ufundi la Tenerife kukubali kipaji na uwezo wake.
  “Kwa mfano kama nilivyokuwa nyumbani nilizoea kupokea mpira na kuutuliza na kutulia nao, huku hairuhusiwi hiyo, ni kupokea na kuachia. Na siyo kuachia tu kutoa pasi za kuipeleka timu mbele kwa kasi,”amesema Farid.
  “Ikitokea umepokea akaja mtu kukukaba, unatakiwa kumpiga chenga au kumtoka kwa haraka na kutoa pasi au kupiga krosi, huku hakuna kuzubaa na mpira, au kuremba sijui kuwafurahisha mashabiki,”ameongeza.
  Farid Mussa kabla ya kuanza mazoezi na wenzake wa Tenerife leo   Mchezaji huyo wa klabu bingwa Afrika Mashariki na Katik, Azam FC amesema kwamba anaanza kuzoea mfumo huo wa uchezaji wa Hispania wa kasi na kutozubaa na mpira.
  “Yaani huku natakiwa kabla sijapata mpira niwe najua nikiupata naufanyia nini kwa manufaa ya timu, ni vitu vidogo vidogo, lakini muhimu sana, naomba Mungu nifanikiwe,”amesema Farid.
  Tangu jana Farid anafanya mazoezi na timu ya kwanza ya Tenerife, baada ya siku tatu za awali kufanya mazoezi na kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 18 cha timu hiyo.
  Mmoja wa Wajumbe wa bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC, Yussuf Bakhresa ambaye yuko Tenerife kwa ajili ya kufuatilia kwa karibu majaribio ya Farid, amesema anafurahia jitihada za mchezaji huyo waliyempandisha kutoka akademi yao mwaka jana.
  Farid Mussa ndani ya Hispania

  “Anaendelea vizuri kwa kweli, nasikia faraja kumuona anachokifanya, namuombea Mungu tu kwa kweli, akifanikiwa yeye atafungua milango ya vijana wengine wengi wa nyumbani,”amesema Yussuf Bakhresa akizungumza na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE leo.
  Awali, Farid ilikuwa apelekwe moja ya klabu za Ligi Kuu ya Hispania, maarufu kama La Liga, kati ya Las Palmas na Athletic ya Bilbao kwa majaribio, lakini wakala wake akashauri mchezaji huyo aanzie timu ya Daraja la Kwanza Hispania ili kupata nafasi ya kucheza na kuinuka haraka.
  Farid alikwenda Hispania Alhamisi iliyopita akitoka kuichezea klabu yake, Azam FC katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Esperance walioshinda 3-0 mjini Tunis Jumanne.
  Farid alifunga bao la kwanza na kuseti la pili lililofungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam dhidi ya Esperance Azam FC ikitoka nyuma kwa 1-0 na kushinda 2-1.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FARID MUSSA: HISPANIA KUGUMU, LAKINI NAKOMAA HADI KIELEWEKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top