• HABARI MPYA

  Friday, April 22, 2016

  JULIO 'ALIWAHISHA' JINA LA MWADUI CAF

  Na Somoe Ng’itu, DAR ES SALAAM
  KOCHA mcheshi, Jamhuri Kihwelo amewaambia TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kupeleka kabisa jina la Mwadui FC makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ajili ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
  Jamhuri, maarufu kwa jina la utani Julio amesema kwamba hiyo inatokana na yeye na timu yake kujiamini watatwaa ubingwa wa TFF, maarufu kama Kombe la Azam Sports Federations Cup (ASFC) 2016 hivyo kupata nafasi ya kucheza Kombe la Shirikisho.
  Mwadui ya Julio itamenyana na Azam FC katika Nusu Fainali ya Kombe la ASFC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga Aprili 24, mwaka huu na mshindi atakutana na mshindi kati ya Coastal Union na Yanga katika fainali.
  Kocha wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema TFF wapeleke jina la timu yake kabisa CAF

  Na Julio amesema kwamba ana historia nzuri katika michuano hiyo baada ya awali kubeba Kombe hilo mara mbili mfululizo akiwa na Tanzaania Stars mwaka 1996 na 1997 na sasa anataka alibebe kwa mara ya tatu akiwa na Mwadui FC.
  Julio amesema kwamba hatishwi hata kidogo na Azam FC wala Yanga, vigogo waliobaki kwenye michuano hiyo baada ya kutolewa kwa Simba SC. “Napiga Azam, na wakija Yanga au Coastal, napiga yeyote, nabeba ndoo, mimi nakuambia TFF wasichelewe, wapeleke kabisa jina la Mwadui Cairo,”amesema Julio. 
  Mwadui FC ilitinga Nusu Fainali baada ya kuitoa Geita Gold kwa kufunga 3-0 katika Robo Fainali, wakati Azam FC iliwatoa Prisons kwa kuwafunga mabao 3-1. 
  Pamoja na kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani, Bingwa wa Kombe la ASFC, michuano iliyoanza na timu 64 Novemba mwaka jana atapatiwa kitita cha Sh. Milioni 50 baada ya Fainali inayotarajiwa kuchezwa wiki moja baada ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kumalizika.
  Mara ya mwisho michuano hiyo ilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu ikaifunga Baker Rangers ya Magomeni katika fainali, wakati ikijulikana kama Kombe la FAT (Chama cha Soka Tanzania). Michuano hiyo imerejea mwaka huu kwa udhamini wa Sh. Bilioni 3.3 wa Azam TV.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: JULIO 'ALIWAHISHA' JINA LA MWADUI CAF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top