• HABARI MPYA

  Saturday, April 30, 2016

  YANGA HAIKAMATIKI BWANA WEE, TOTO YAFA 2-1 KIRUMBA….UBINGWA NJIA MOJA JANGWANI

  Na Prince Akbar, MWANZA
  YANGA SC imezidi kupaa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kufuatia ushindi wa 2-1 dhidi ya wenyeji Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
  Ushindi huo unaifanya Yanga ifikishe pointi 65 baada ya kucheza mechi 26, ikiendelea kuongoza Ligi Kuu, mbele ya Azam FC na Simba SC.
  Haikuwa rahisi kwa Yanga leo kuondoka na pointi tatu mjini Mwanza, kwani ililazimika kutoka nyuma kwa 1-0 na kuibuka na ushindi huo, baada ya William Kimanzi kutangulia kuifungia Toto dakika ya 39 kwa kichwa akimalizia kona ya Abdallah Seseme.

  Baada ya bao hilo, wachezaji wa Yanga walijitahidi kucheza kwa nguvu ili kupata bao la kusawazisha kabla ya dakika 45 za kipindi cha kwanza, lakini ukuta wa Toto ukiongozwa na Karlos Protus ulizuia mashambulizi ya wachezaji wa Yanga.
  Juhudi za washambuliaji hatari wa Yanga, Donald Ngoma, Simon Msuva na Amissi Tambwe ziligonga ukuta hadi mwamuzi Ludovick Charles kutoka mkoani Kagera alipopuliza filimbi ya mapumziko.
  Kipindi cha pili kilianza pasipo timu yoyote kufanya mabadiliko hadi dakika 50, Tambwe alipoisawazishia Yanga.
  Bao hilo liliwaamsha zaidi wachezaji wa Yanga baada ya kulishambulia lango la wapinzani wao mara kwa mara hali iliyompa wakati mgumu kipa wa Toto, Mussa Mohamed kuokoa sekeseke langoni mwake.
  Shambulizi la kushitukizwa lililofanywa na washambuliaji waYanga, lilisaidia kuipatia timu hiyo ya mtaa wa Jangwani jijini Dar es Salaam, bao la ushindi lililofungwa na beki wa kulia, Juma Abdul dakika 78.
  Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Vincent Bossou, Haruna Niyonzima/Thabani Kamusoko, Salum Telela, Simon Msuva, Amissi Tambwe/Malimi Busungu, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Matheo Anthony.
  Toto Africans; Mussa Mohamed, Eric Muliro, Hassan Khatibu, Salum Chukwu, Carlos Protus, Jamal Soud, Abdallah Seseme, Waziri Junior, William Kimanzi na Edward Christopher.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA HAIKAMATIKI BWANA WEE, TOTO YAFA 2-1 KIRUMBA….UBINGWA NJIA MOJA JANGWANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top