• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 26, 2016

  AZAM NA YANGA WATENGEWA VIPORO VYAO TENA KESHO, CHA NANI KITACHACHA?

  RATIBA LIGI KUU YA VODACOM TZ BARA MWEZI HUU
  Leo; Aprili 27, 2016
  Azam FC Vs Majimaji
  Yanga SC Vs Mgambo JKT
  Aprili 30, 2016
  Toto Africans Vs Yanga SC
  African Sports Vs Coastal Union
  Mwadui FC Vs Stand United
  Mtibwa Sugar Vs Mbeya City
  Prisons Vs JKT Ruvu
  Kikosi cha Azam FC kesho kitakuwa Uwanja wa nyumbani, Chamazi dhidi ya Majimaji

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea kesho kwa michezo miwili, yote Dar es Salaam.
  Azam FC watakuwa wenyeji wa Majimaji ya Songea Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, wakati Yanga watakuwa wenyeji wa Mgambo JKT, Uwanja wa Taifa, eneo la Mgulani. 
  Yanga na Azam wote wanaingia kwenye michezo hiyo wakitoka kwenye mechi za Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) mwishoni mwa wiki na mechi za michuano ya Afrika katikati ya wiki.
  Azam FC Jumanne ilifungwa 3-0 na Esperance ya Tunisia mjini Tunis katika mchezo wa 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kushinda 2-1 Chamazi.
  Yanga SC Jumatano ilifungwa mabao 2-1 na Al Ahly ya Misri mjini Alexandria katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Hata hivyo, wakati Azam imeaga moja kwa moja michuano hiyo, Yanga itamenyana Sagrada Esperanca ya Angola kuwania kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.
  Jumapili Azam FC iliifunga Mwadui FC kwa penalti 5-3 baada ya sare ya jumla ya 2-2 ndani ya dakika 120 katika Nusu Fainali ya Kombe la ASFC. 
  Mechi kati ya Yanga na Coastal ilivunjika dakika ya 110 baada ya mashabiki kumjeruhi kwa jiwe mshika kibendera namba mbili, Charles Simon wa Dodoma, wageni wakiwa wanaongoza kwa mabao 2-1.
  Yanga SC wataikaribisha Mgambo JKT kesho Uwanja wa Taifa

  Ni matarajio Yanga watacheza fainali na Azam FC mwezi ujao baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu. 
  Kocha Mholanzi wa Yanga SC, Hans van der Pluijm ataendelea kumkosa beki wake chaguo la kwanza upande wa kushoto, Mwinyi Hajji Mngwali ambaye ni majeruhi.
  Lakini hana wasiwasi Oscar Joshua Fanuel ataendelea kuziba pengo hilo kama ambavyo amekuwa akifanya katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Al Ahly mjini Cairo na Coastal Union mjini Tanga.
  Kocha Muingereza, Stewart Hall ambaye ataendelea kuwakosa mabeki Shomary Kapombe, Serge Wawa na mshambuliaji Kipre Tchetche ambao ni majeruhi na winga Farid Mussa aliyekwenda kwenye majaribio Hispania, kesho atakutana na mwanafunzi wake wa ukocha, Kali Ongala. 
  Stewart alimstaafisha soka Kali Azam FC na kumuhamishia kwenye benchi la Ufundi mwaka 2011 ambako baada ya miaka mitatu aliondoka na sasa yuko Majimaji kama kocha Mkuu.
  Hadi sasa, Yanga SC inaongoza mbio za ubingwa kwa pointi zake 59 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na watani wao wa jadi, Simba SC wenye pointi 57 za mechi 25, wakati Azam FC yenye pointi 55 zamechi 24 ni ya tatu.  
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: AZAM NA YANGA WATENGEWA VIPORO VYAO TENA KESHO, CHA NANI KITACHACHA? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top