• HABARI MPYA

  Jumapili, Aprili 24, 2016

  RIPOTI ZOTE ZAIPELEKA YANGA FAINALI KOMBE LA ASFC

  Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
  RIPOTI za waamuzi na Kamisaa wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup kati ya wenyeji, Coastal Union na Yanga na Dar e Salaam zimetua TFF.
  Na habari za ndani ambazo BIN ZUBEIRY SPORTS SPORTS – ONLINE imezipata zinasema ripoti hizo zimeipeleka Yanga fainali baada ya mchezo kuvunjika dakika ya 110 jioni ya leo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
  Mchezo huo ulivunjika wakati Yanga ikiwa mbele kwa mabao 2-1 kufuatia mshika kibendera namba mbili, Charles Simon kupasuliwa juu ya jicho la kushoto kwa jiwe lililotupwa na shabiki.
  Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga, Donald Ngoma (kulia) akiwania mpira dhidi ya beki wa Coastal, MIraj Adam

  “Ripoti zote, ya marefa na kamisaa zinaonyesha mashabiki waliofanya fujo ni wa Coastal, maana yake Coastal ndiyo wanapoteza mchezo na Yanga inakwenda fainali,”kimesema chanzo.
  Coastal Union ilitangulia kwa bao la kiungo Mcameroon, Youssouf Sabo kabla ya Yanga kusawazisha kupitia kwa mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma, mabao yote kipindi cha pili.
  Mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe akaifungia Yanga bao la pili mwanzoni tu mwa dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1.
  Baada ya bao hilo, mchezo ukasimama dakika ya 105 kufuatia mashabiki wanaodaiwa kuwa ni wa Coastal kuanza kutupa chupa na mawe uwanjani na kumjeruhi mshika kibendera namba mbili, Charles Simon juu ya jicho la kushoto. 
  Refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga akapuliza kipyenga cha kuhitimisha mchezo huo dakika ya 110, huku mashabiki wakiendelea kuushambulia uwanja kwa mawe na chupa.
  Kamisaa wa mechi, Osuri Kosuri kutoka Simiyu alisema kuwa wamelazikika kuvunja mchezo kufuatia vurugu zilizotokea uwanjani. 
  Kosuri alisema kuwa Usalama ulikuwa mdogo uwanjani hapo na askari walishindwa kuhimili vurugu. 
  Iwapo Yanga itapewa ushindi, itamenyana na Azam FC katika fainali mwezi ujao. Azam leo imeitoa Mwadui FC kwa penalti 5-3 kufuatia sare ya 2-2 baada ya dakika 120 Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: RIPOTI ZOTE ZAIPELEKA YANGA FAINALI KOMBE LA ASFC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top