• HABARI MPYA

  Jumatatu, Aprili 25, 2016

  SAMATTA KUFANYIWA VIPIMO KESHO BAADA YA KUJERUHIWA PUA UBELGIJI

  Na Mwandishi Wetu, GENK
  MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta kesho anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya pua baada ya kuumia jana katika mchezo wa mchujo wa kuwania kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao. 
  Samatta alicheza kwa dakika 45 tu za kwanza jana, wakati timu yake, KRC Genk ikifungwa 2-1 na Gent katika mchezo wa mchujo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji kuwania kucheza michuano ya Ulaya, tena Uwanja wa nyumbani, Cristal Arena mjini Genk.
  Samatta alitolewa baada ya kumalizika kipindi cha kwanza, akimpisha mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis ambaye wamekuwa wakipokezana siku zote.
  Na baadaye Genk ikasema Samatta aliumia pua ndiyo maana akashindwa kuendelea na mchezo.
  Samatta mwenyewe leo amesema kwamba alisikia maumivu makali na kizunguzungu baada ya kugongana na mchezaji wa Genk, hivyo akaona apumzike.
  Samatta amesema kesho atafanyiwa vipimo ili kujua ameumia kiasi gani.
  Mbwana Samatta wa mbele akiingia uwanjani kwenye mchezo wa jana
  Mbwana Samatta (wa tatu kushoto) akiwa kwenye mstari wa wachezaji wa wa Genk jana kabla ya mchezo
  Mbwana Samatta (chini) akipiga mpira nyuma ya mchezaji wa Gent jana
  Mbwana Samatta (kulia) akishangilia na wachezaji wenzake baada ya kupata bao jana
  Samatta alitoka jana timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, Genk wakitangulia kwa bao la Leon Bailey dakika ya 16, kabla ya Laurent Depoitre kuwasawazishia wageni dakika ya 23. 
  Renato Neto akaifungia Gent bao la ushindi kwa penalti dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90 za kawaida za mchezo.
  Huo ulikuwa mchezo wa 11 tangu ajiunge na Genk Januari mwaka huu akitokea TP Mazembe ya DRC, akiwa amefunga mabao nne. 
  Samatta alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem mwishoni mwa wiki baada ya awali kufunga katika ushindi wa 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende na 3-2 dhidi ya Club Brugge.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: SAMATTA KUFANYIWA VIPIMO KESHO BAADA YA KUJERUHIWA PUA UBELGIJI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top