• HABARI MPYA

  Jumatano, Aprili 27, 2016

  UBINADAMU WA MAREFA UNAPOZIDI, HAYO NDIYO MATOKEO YAKE!

  MAAMUZI ya ovyo ya marefa yameshuhudiwa mwishoni mwa wiki katika Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation Cup (ASFC) baina ya wenyeji, Coastal Union na Yanga ya Dar es Salaam mjini Tanga.
  Mchezo huo ulivunjika dakika ya 110, kufuatia mwamuzi msaidizi namba mbili, Charles Simona wa Dodoma kujeruhiwa kwa jiwe lililorushwa na mashabiki, wakati huo Yanga wakiongoza kwa mabao 2-1.
  Na mashabiki hao ambao wazi walikuwa ni wa timu mwenyeji, walifikia hatua ya kumshambulia mwamuzi huyo baada ya kukerwa na maamuzi yake yasiyo ya kujiamini na ambayo yalionekana kuiumiza timu yao.

  Kwanza ilikuwa ni katika bao la kwanza la Yanga lililofungwa na mshambuliaji Mzimbabwe, Donald Ngoma ambalo lilikuwa la kusawazisha baada ya Coastal kutangulia kwa bao la kiungo Mcameroon, Youssouf Sabo, kipindi hicho hicho, cha pili.
  Ilionekana kama Ngoma alikuwa amezidi wakati anakwenda kufunga, na Simon alinyoosha kibendera kuashiria ni hivyo, lakini refa Abdallah Kambuzi wa Shinyanga akarudisha mpira katikati, kuashiria lilikuwa ni bao halali. Wachezaji wa Coastal walimzonga mwamuzi huyo kwa sekunde kadhaa kabla ya kukubali matokeo na kuanza mchezo.
  Katika dakika 30 za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1, Yanga wakapata bao la pili, sina shaka kusema halikuwa bao halali, kwani mfungaji Amissi Tambwe alionekana kabisa kuudondeshea mpira nyavuni kwa mkono.
  Charles Simon hakuwa na maamuzi yoyote juu ya bao hilo, alikuwa amesimama tu na kibendera chake bila ya kuondoka eneo alilokuwa. Angeondoka, kuelekea katikati angemaanisha ni bao. Na kwa kutoondoka bila hata kunyoosha kibendera ndiyo utata wenyewe na hilo ndilo lililowakera mashabiki wa Coastal na kuanza kumrushia mawe.
  Niungane na wanamichezo wengine kulaani vurugu zilizotokea na hususan kushambuliwa kwa waamuzi.
  Mara nyingi tumekuwa tukijaribu kupoza hasira za mashabiki juu ya makosa ya marefa, kwa kusema na wao ni binadamu, kukosea si ajabu.
  Lakini huo ubinadamu wa marefa wa kukosea kukosea unapozidi, matokeo yake ni vurugu hata watu kuuawa viwanjani mara kadhaa imeshuhudiwa.
  Hiyo ilimfanya hadi Rais wa zamani wa FIFA, Sepp Blatter wakati fulani, aseme soka na vurugu ni chanda na pete – na ni kweli kwa sababu mashabiki wanaongozwa na hisia.
  Hivyo basi ni muhimu wakati wote kuhakikisha tunaweka mechi katika mazingira salama ya tahadhari pia, jambo ambalo halikuwepo Mkwakwani Jumapili.
  Haikuwa mara ya kwanza mashabiki kufanya vurugu zenye kuhatarisha amani Uwanja wa Mkwakwani, bali imekuwa ni kawaida sasa, lakini ajabu bado mazingira hayajaboreshwa na tahadhari zimekuwa si za kutosha.
  Uzio wa Uwanja na majukwaa ya Mkwakwani vipo karibu mno na si ajabu mara kwa mara wachezaji na hata marefa wamekuwa wakishambuliwa.
  Mapema tu siku hiyo kabla ya mchezo kuvunjika kwa sababu refa alipigwa jiwe, lakini ungeweza kuvunjika kabla baada ya mashabiki kumrushia chupa za maji kipa wa Yanga, Deo Munishi ‘Dida’.
  Bahati nzuri askari Polisi walikwenda na kuwatuliza mashabiki hao wanaoketi nyuma ya lango Kaskazini ambao kwa uzoefu wangu ndiyo huongoza kwa vurugu.
  Ni kweli baadhi ya matatizo katika soka yetu yanaonekana si ya kwisha karibuni, mfano la miundo mibovu ya viwanja – ila suala la waamuzi kuchezesha ovyo halina sababu ya kuendelea kuwapo.
  Kufungia tu waamuzi haisadii iwapo TFF haitafanya jitihada za ziada kuhakikisha inakuwa na marefa ambao watafanya kazi yao vizuri na hata yakitokea mapungufu, basi yachukuliwe kuwa ni kweli ya kibinadamu na zisiwepo hisia nyingine.
  Tuwapongeze askari Polisi waliokuwapo Uwanja wa Mkwakwani kwa kufanikisha kuwaondoa mashabiki uwanjani jambo ambalo lilisaidia kutotokea athari zaidi, lakini ukweli ni kwamba madudu ya waamuzi siku hiyo ndiyo yalikuwa chanzo cha vurugu. 
  Suala si bao la kuotea wala la mkono – kwani yote hayo si mambo mageni kwenye ulimwengu wa soka – hata hao Yanga wamekwishafungwa mabao ya mkono na kuzidi pia kabla na baada ya Diego Maradona kuwafunga bao la ‘Mkono wa Mungu’ England katika Kombe la Dunia mwaka 1986.
  Tatizo ni marefa kukosea kibinadamu dhidi ya timu moja tu uwanjani – jambo ambalo lilijenga hisia kwa mashabiki wa Coastal kwamba wanaonewa. 
  Marefa ambao walipitiwa kumtoa kwa kadi nyekundu beki wa Yanga, Oscar Joshua kwa kumrudishia pigo beki wa Coastal, Hamad Juma ndiyo hao hao ambao walilikubali bao la mkono la wageni, unategemea nini?
  Na Marefa ambao walimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Coastal Adeyoum Ahmed kwa kuushika mpira, ndiyo marefa ambao hawakuwa wanaona makosa ya wachezaji wa Yanga uwanjani, ikiwemo faulo ambayo Kevin Yondan alimchezea Mbwana Khamis 'Kibacha' kabla ya Ngoma kuifungia timu yake bao la kusawazisha.
  Ajabu pamoja na matukio ya kihistoria ya kuvunjika kwa amani uwanjani baada ya madudu ya marefa, likiwemo la
  refa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Abdulkadir Omar ‘Msomali’ kuruhusu bao la mkono Machi 31, 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikiifunga Yanga 4-1, bado hatujajifunza.
  Mechi hiyo iliyohudhuriwa na rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka kufunga bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa. 
  Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za maji na mashabiki wa Yanga. 
  Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa na FFU ndipo akaendeleza mchezo na Yanga ikafa 4-1 Shamba la Bibi.
  Na tena bao la mkono la Madaraka lililokuwa la pili dakika ya 32 baada ya timu hizo kuwa zimefungana 1-1, Simba wakitangulia kwa bao la Mkenya Mark Sirengo na Sekilojo Chambua kuisawazishia Yanga dakika ya 16, ndilo liliwaondoa mchezoni Yanga wakaruhusu mawili zaidi. Mabao mengine ya Simba yalifungwa na Sirengo dakika ya 76 na Emmanuel Gabriel dakika ya 83.
  Kwa mara nyingine katika soka ya Tanzania tumejionea nini hufuatia makosa ya kibinadamu ya marefa yanapozidi – je tumejifunza nini? 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: UBINADAMU WA MAREFA UNAPOZIDI, HAYO NDIYO MATOKEO YAKE! Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top