• HABARI MPYA

  Jumanne, Aprili 26, 2016

  HAYA NDIYO MAPUNGUFU YA YANGA KWA MUJIBU WA KADITO

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  YANGA SC imeshauriwa kutafuta video za mechi zake zote dhidi ya APR ya Rwanda na Al Ahly ya Misri katika Ligi ya Mabingwa Afrika ili kutazama mapungufu yake, kabla ya kwenda Kombe la Shirikisho.
  Jumatano Yanga ilitolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika na Al Ahly ya Misri kwa jumla ya mabao 3-2, baada ya kufungwa 2-1 Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora, kufuatia kulazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
  Yanga ilianza vizuri ikicheza mechi zake nne za awali bila kupoteza hata moja, ikishinda tatu na kutoa sare moja.
  Yanga ilishinda 1-0 dhidi ya Cercle de Joachim nchini Maurtius na 2-0 Dar es Salaam katika mchujo wa awali, kabla ya kushinda 2-1 Kigali dhidi ya APR na kutoa sare ya 1-1 Dar es Salaam.
  Dennis Kadito (kushoto) akiwa Uwanja wa Signal Iduna Park wa Borussia Dortmund nchini Ujerumani

  Sasa mabingwa hao wa Tanzania watamenyana na Sagrada Esperanca ya Angola kuwania kuingia kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mwezi ujao.
  Mchezo wa kwanza umepangwa kufanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kati ya Mei 6 na 8 wakati wa marudiano utafanyika Angola kati ya Mei 17 na 18.
  Na Dennis Kadito, Mtanzania na mdau wa soka anayeishi Uholanzi alitazama mechi zote za Yanga dhidi ya APR na Ahly na kugundua mapungufu kadhaa, ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi haraka.
  Katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY SPORTS – ONLINE jana, Kadito anayewasaidia wachezaji wa Afrika Mashariki na Kati kupata timu Ulaya na nchi nyingine za Afrika zilizopiga hatua kisoka, amesema katika mchezo wa mwisho na Ahly Yanga walikuwa wana ari ya kucheza kwa kujilinda kitimu.
  Hata hivyo, akasema uchezaji wao haukuwa mzuri kulinganisha na viwango vya timu nyingine kwenye michuano hiyo, kwamba Yanga bado ina mapungufu makubwa.
  “Mchezaji wa Al Ahly akipata mpira, tayari ana hesabu mbili au tatu za kugawa mpira. Mchezaji wa Yanga anapokuwa na mpira anakuwa na hesabu moja au hana kabisa. Matokeo yake hakuna pasi za mwendelezo,”amesema Kadito.
  “Mtu akiangalia mechi bila ushabiki, ataona tuna mapungufu mengi bado na tatizo kubwa ni wachezaji wetu. Sababu mwalimu (Mholanzi Hans van der Pluijm) unaona anafanya kazi na Yanga wamebadilika kama timu,”.
  “Angalia (Thabani) Kamusoko (Mzimbabwe) japokuwa umri umekwenda, lakini anavyocheza ni tofauti sana na viungo wetu (Watanzania), au mwangalie (Simon) Msuva, ana miaka mingapi? Acha tunayoijua Watanzania. Sasa mchezaji kama huyo bado anafanya makosa yale yale miaka yote, krosi hazina macho, utamlaumu kocha?”.
  Kadito aliyempeleka beki Shomary Kapombe AS Cannes ya Ufaransa mwaka juzi kabla ya mchezaji huyo mwenyewe kuamua kurudi nyumbani kujiunga na Azam FC, amewashauri Yanga waangalie video za mechi zao na Al Ahly na APR ili wafanyie kazi mapungufu,”
  “Katika mechi na Ahly, Yanga wamefungwa kizembe, kwa sababu wachezaji hawajipangi vizuri. Hesabu wachezaji wanaozuia dhidi ya wanaoshambulia, wanakosea mno,” anasema. Kadito aliyemsaidia mshambuliaji wa Burundi, Abdul Razak Fiston kununuliwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini mwaka jana, amesema kwamba tatizo hilo lipo hata kwa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
  “Suala kubwa ni kujipanga, nina uhakika kocha anafanya kazi yake, itakuwa ni matatizo ya wachezaji wetu tu. Na katika kutatua hili, kuna mipango ya muda mfupi na muda mrefu, kwa muda mfupi ni kocha kurudia mafunzo yake, lakini pia apatikane mtaalamu (psychologist) wa kuwaweka wachezaji sawa. Zaidi ya hapo hakuna sayansi zaidi,” anasema.
  Kadito (kulia) akiwa na mchezaji wa kimataifa wa Burundi, Abdul Razak Fiston wakati anamsaidia kujiunga na Mamelodi Sundowns
  Kadito akiwa na mtoto wa dada yake, Thomas  van der Schaaf anayechezea timu ya vijana chini ya umri wa miaka nane (U-8)

  Kwa mipango ya muda mrefu, Kadito anashauri Yanga kuanzisha akademi ya soka ya vijana wadogo walelewe vizuri katika misingi ya soka. “Mimi niko huku, naona tofauti, vijana wanabadilika na wanakuwa na maarifa kichwani jinsi ya kujipanga. Ukiangalia video za Yanga na Ahly, unaona hao Waarabu wanapanga shambulizi tokea nyuma hadi mbele. Yaani kama mtazamaji unaona mpira unaelekea vipi, Yanga mashambulizi yao ya kuungaunga,” anasema.
  Na Kadito anaongeza kwamba Yanga hawapaswi hata kufikiria kubadili kocha kwa sababu tatizo makocha Wazungu wanaletwa kufundisha watu wazima vitu vya awali kabisa katika mafunzo ya soka.
  “Mtu ana miaka 20 unamfundisha jinsi ya kujipanga? Ndio maana nikasema ni tatizo la wachezaji na nikatoa mfano wa Msuva na Kamusoko. Umeona Kamusoko anavyojipanga? Mara nyingi ana hesabu za kutoa pasi kwa watu wawili au watatu. Hii ni akili ya mpira na ya kufundishwa,”.
  Thabani Kamusoko (kushoto), mchezaji anayemvfutia Kadito akiwania mpira dhidi ya kiungo wa Coastal Union, Dk. Ayoub Yahya juzi mjini Tanga

  “Ndiyo maana mchezaji wa Kiafrika akizidi miaka 20 vigumu kumleta Ulaya. Siyo kwamba hana kipaji, ni kwamba kiufundi amechelewa. Labda niseme kwamba, naona Azam watafika mbali miaka miwili au mitatu ijayo zaidi ya Yanga au Simba,”anasema.
  “Mtu kama Msuva kapitia makocha wangapi, lakini bado anafanya makosa yale yale? Hili tatizo la kocha au mchezaji zaidi? Mimi namfuatilia Msuva kwa miaka minne, Juma Abdul namkubali, ila nadhani umri umeenda,”anasema.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: HAYA NDIYO MAPUNGUFU YA YANGA KWA MUJIBU WA KADITO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top