• HABARI MPYA

  Alhamisi, Aprili 21, 2016

  FARID AONDOKA LEO TUNIS KWENDA KUJARIBU BAHATI LA LIGA

  Na Princess Asia, TUNIS
  WINGA wa Azam FC, Farid Mussa anatarajiwa kuondoka leo mjini Tunis, Tunisia kwenda Hispania kwa ajili ya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa.
  Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE jana kwamba Farid atakuwa na majaribio katika klabu mbili na baada ya hapo, wakala wake ataamua aende timu gani.
  Kawemba amezitaja timu hizo kuwa ni Union Deportiva Las Palmas, maarufu kama Las Palmas yenye maskani yake Las Palmas de Gran Canaria na Athletic ya Bilbao.
  Farid Mussa anaondoka leo kwenda Hispania kwa majaribio ya wiki mbili

  “Kwa mujibu wa wakala wake, anasema amempatia nafasi mbili za majaribio katika klabu mbili zote za La Liga na anatarajiwa kuondoka baada ya mchezo wetu na Esperance hapa,”amesema Kawemba.
  Farid anaondoka na maumivu baada ya juzi kuumia akiichezea Azam FC katika mchezo wa marudiano hatua ya 16 Bora Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji, Esperance walioshinda 3-0 mjini Tunis.
  Kawemba amesema Farid aliyefunga bao la kwanza na kuseti la pili lililofungwa na Ramadhani Singano ‘Messi’ katika mchezo wa kwanza mjini Dar es Salaam Azam FC ikitoka nyuma kwa 1-0 na kushinda 2-1 anatarajiwa kuwa Hispania kwa wiki mbili.
  “Kwa kuanzia atakuwa kule kwa wiki mbili, hiyo ni kwa ajili ya majaribio tu, lazima kila klabu ipate muda wa kutosha wa kumtazama na baada ya hapo, tutapewa majibu,”amesema.
  Kikosi cha Azam FC kinaondoka leo pia kurejea Dar es Salaam na Jumapili kitakuwa na mchezo wa ugenini dhidi ya Mwadui FC mkoani Shinyanga katika Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Azam Sports Federation Cup (ASFC). 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: FARID AONDOKA LEO TUNIS KWENDA KUJARIBU BAHATI LA LIGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top