HABARI MOTOMOTO

HABARI ZA NYUMBANI

HABARI ZA KIMATAIFA

HABARI ZA AFRIKA

MAKALA

SANAA NA BURUDANI

NGAO YA JAMII ENGLAND

SUPER CUP YA UJERUMANI

Style28

SHERMAN NA NGASSA USO KWA USO JUMAMOSI LIGI KUU AFRIKA KUSINI

FREE State Stars yenye Mrisho Khalfa Ngassa na Black Aces yenye Kpah Sean Sherman zitakutana Jumamosi katika mchezo wa fungua dimba ya Ligi Kuu ya ABSA Afrika Kusini.
Free State ndiyo watakuwa wenyeji wa Blac Aces Uwanja wa Ground Goble Park mjini Bethlehem siku hiyo.
Wawili hao, Sherman na Ngassa wote walikuwepo katika kikosi kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na Yanga SC msimu uliopita kabla ya kuhamia Afrika Kusini msimu huu. 
Kwa mujibu wa ratiba ya msimu wa PSL wa 2015-16, mabingwa watetezi, Kaizer Chiefs wataanza kutetea taji lao dhidi ya Chippa United Agosti, Mamelodi Sundowns na Platinum Stars, Orlando Pirates na SuperSport United, wakati timu mbili zilizopanda msimu huu, Golden Arrows na Jomo Cosmos watakuwa nyumbani na University ya Pretoria na ugenini na Maritzburg United.
Mechi ya pili, Ngassa kushoto atakutana na mabingwa wa ABSA, Kaizer Chiefs.
Sherman baada ya kujiunga na Free State Stars 

RATIBA YA MECHI ZA UFUNGUZI LIGI KUU AFRIKA KUSINI
Free State Stars vs Black Aces
Polokwane City vs Bloem Celtic
Platinum Stars vs Mamelodi Sundowns
Chippa United vs Kaizer Chiefs
Bidvest Wits vs Ajax Cape Town
Golden Arrows vs AmaTuks
SuperSport vs Orlando Pirates
Maritzburg United vs Jomo Cosmos
Mrisho Ngassa baada ya kutua Free State Stars

RAUNDI YA PILI LIGI KUU YA ABSA
Raundi ya Pili ya Ligi Kuu ya Absa
Orlando Pirates vs Chippa United
Ajax Cape Town vs Maritzburg United
AmaTuks vs Polokwane City
Black Aces vs SuperSport United
Kaizer Chiefs vs Free State Stars
Mamelodi Sundowns vs Bidvest Wits
Bloem Celtic vs Platinum Stars
Jomo Cosmos vs Golden Arrows

‘LIGI KUU NDOGO’ KUPIGWA KAMBARAGE KUANZIA JUMAMOSI

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
CHAMA cha Soka Shinyanga (SHIREFA), kwa kushirikiana na kampuni ya Cleverland Res ya Mwanza, wameandaa mashindano maalum ya timu za Ligi Kuu za Kanda ya Ziwa Victoria.
Mratibu wa mashindano hayo, Kabole Kahungwa ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo kwamba michuano hiyo itashirikisha timu zote za Kanda ya Ziwa zilizopo Ligi Kuu na yatafanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.
Amezitaja timu hizo kuwa ni Stand United, Mwadui FC zote za Shinyanga, Toto African ya Mwanza na Kagera Sugar ya Bukoba.
Kikosi cha Stand United kilichoshiriki Ligi Kuu msimu uliopita

Kahungwa, mchezaji wa zamani wa Pamba ya Mwanza na Simba SC ya Dar e Salaam amesema mashindano hayo ni maalum kwa ajili ya kuzipa maandalizi timu za Kanda ya Ziwa kabla ya Ligi Kuu.
“Kama unavyoona timu za Kanda ya Ziwa zimefanya usajili mzuri kuelekea Ligi Kuu, kwa hivyo na sisi tukaona tuziandalie mashindano baina yao ili kujiweka fiti,”amesema Kahungwa.
Ligi Kuu inatarajiwa kuanza wiki ya pili ya Septemba na Kanda ya Ziwa msimu huu itakuwa na nne, kutoka mbili za msimu uliopita Kagera Sugar na Stand United, baada ya kupanda kwa Toto na Mwadui.

AGOSTI 8, 2015
Stand United Vs Mwadui FC
AGOSTI 9, 2015
Toto African Vs Kagera Sugar
AGOSTI 10, 2015
Mwadui FC Vs Toto Africans
AGOSTI 11, 2015
Kagera Sugar Vs Stand United
AGOSTI 12, 2015
Stand United Vs Toto African
AGOSTI 13, 2015
Mwadui FC Vs Kagera Sugar

ZUTTAH, COUTINHO WATUPIWA VIRAGO YANGA SC, BEKI MTOGO, MIDO LA ZIMBABWE MBIONI KUTUA JANGWANI

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
BEKI Mghana Joseph Tetteh Zutah na kiungo Mbrazil Andrey Coutinho wanaweza kutemwa Yanga SC kupisha wachezaji wengine kabla ya dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa wiki.
Dirisha la usajili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara linatarajiwa kufungwa Agosti 6, mwaka huu na baada ya hapo kutakuwa na nafasi ya kusajili wa wachezaji huru tu kwa wiki moja ya mwisho kabla ya kuanza msimu mpya. 
Baada ya Yanga SC kutolewa katika Robo Fainali michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame imekitathmini kikosi chake na kugundua Zuttah na Coutinho hawana faida.
Joseph Tetteh Zuttah (kulia) na Andrey Coutinho (kushoto) wote wapo hatarini kutemwa Yanga SC

Coutinho alijiunga na Yanga SC msimu uliopita akiletwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Mbrazil mwenzake, Marcio Maximo na hadi sasa ameichezea timu hiyo mechi 33 na kuifungia mabao sita.
Mbrazil huyo alikuwa ana wakati mzuri chini ya kocha Maximo, lakini tangu ujio wa Mholanzi, Hans van der Pluijm amepoteza nafasi katika kikosi cha kwanza.
Zuttah amesajiliwa Juni mwaka huu kufuatia kupendekezwa na kocha Pluijm, lakini baada ya wiki mbili za Kombe la Kagame, uongozi umeona hana umuhimu.
Mbali na Sherman, Coutinho na Zuttah wachezaji wengine wa kigeni Yanga SC ni Mkongo, Mbuyu Twite, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima, Mrundi Amissi Tambwe na Mzimbabwe Donald Ngoma.
Yanga SC ilifungwa kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 katika Robo Fainali ya Kagame dhidi ya Azam FC wiki iliyopita na tathmini ya baada ya mashindano, inaonyesha timu inahitaji marekebisho madogo. 
Na kwa kuona uimara wa Azam FC iliyotwaa Kombe la Kagame mwishoni mwa wiki na namna wapinzani, Simba SC wanavyojiimarisha, Yanga SC imeona kuna umuhimu wa kuleta wachezaji wengine bora zaidi kuchukua nafasi za Coutinho na Zuttah.
Nahodha wa FC Platinum ya Zimbabwe kiungo, Thabani Kamusoko, tayari yuko kwenye rada za Jangwani achukue moja ya nafasi hizo mbili. 
Aidha, wakala Mganda, Gibby Kalule aliyewahi kuwauzia Yanga SC, mshambuliaji Mliberia, Kpah Sherman amependekeza beki wa kimataifa wa Togo, Vincent Bossou mwenye umri wa miaka 29 anayechezea Goyang Hi FC ya Korea Kusini.

WAKASO AMFUATA MUNTARI UARABUNI BAADA YA MAMBO KWENDA MRAMA ULAYA

KIUNGO wa kimataifa wa Ghana, Mubarak Wakaso (pichani) amekamilisha uhamisho wake kwenda Al-Ittihad ya Saudi Arabia kwa Mkataba wa miaka mitatu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amefaulu vipimo vya afya jana mjini Milan na mara moja atajiunga na wachezaji wenzake wapya mwishoni mwa wiki.
Wakaso alikuwa katika wakati mgumu katika Ligi ya Urusi kabla ya kwenda kwa mkopo Celtic ya Ligi Kuu ya Scotland msimu uliopita, ambako pia alishindwa kung’ara licha ya kuwa na mwanzo mzuri.
Na Wakaso ametua katika timu hiyo baadab ya kusukiwa mipango na mchezaji mwenzake wa kimataifa wa Ghanam Sulley Muntari, ambaye awali alimpendekeza Kevin-Prince Boateng anayechezwa Schalke 04 kwa sasa lakini akakataa kuondoka Ujerumani.

BEKI MAN UNITED ATUA LYON YA UFARANSA MIAKA MINNE

Beki wa zamani wa kulia wa Manchester United, Rafael da Silva (katikati) amesaini Mkataba wa miaka minne kujiunga na Lyon ya Ufaransa PICHA ZAIDI GONGA HAPA

SHILOLE ANAPOSHINDANA NA SERIKALI INAKUWA KITU FLAN AMAZING

Unapowauliza watu wengi wenye hekima zao pale wanapokuwa na kesi mahakamani, jibu la huwa ni moja tu: “Shauri hili lipo mahakamani, siwezi kulizungumzia kwa sasa.” …Na pale hukumu inapotolewa kinyume na matarajio yao, basi watakuambia “Tunaandaa utaratibu wa kukata rufaa”.
Hivi ndivyo nilivyomtarajia msanii Shilole awe hivyo pale alipofungiwa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kosa la kucheza uchi, ikiwa ni mara yake ya pili kufanya hivyo.
Kwangu mimi nilikuwa namuona Shilole kama msanii mpiganaji, aliyepambana kutoka chini hadi kuwa mmoja mastaa wanaozungumzika kwenye ‘game’ .
Msanii aliyeweza kusaka upenyo wa fursa baada ya kuona nafasi ya kupasua kwenye filamu ni finyu, akapenya kwenye muziki, nyimbo zikasumbua kwenye media, show zikikamiminika, mialiko ya nje ya nchi ikabisha hodi kwa kasi.
Lakini pamoja na upambanaji wake, usasa ulimsumbua Shilole, uvaaji uliokiuka maadili ya kitanzania ikawa ni sehemu ya taratibu zake za kazi, uchezaji uliojaa ukakasi nao pia ukawa ni moja ya ‘silaha’ zake kubwa kwenye kuboresha soko lake.
BASATA ilishamwita Shilole na kumpa karipio kali, mwenye akaomba radhi kwa maandishi, pengine bila yeye kujua kuwa ile ni kadi yake ya njano, bibie huyo akaendelea na ‘swaga’ zake ya kuuanika mwili wake. 
Shilole akawa na onyesho nchini Ubelgiji, akafanya yasiyostahili jukwaani, BASATA wakamwita tena na kwa mara nyingine akaomba radhi kwa njia ya maandishi, baada ya hapo hukumu ikafuata …Shilole akafungiwa kufanya maonyesho ya muziki kwa mwaka mmoja ndani na nje ya nchi.
Na hapo ndipo nilipotegemea busara za Shilole, atambue kuwa Basata si taasisi ya mtu binafsi, BASATA ni chombo rasmi cha serikali, kinachofanya kazi kwa niaba ya serikali na hivyo tamko lolote la BASATA ni sawa na tamko la serikali.
Wakati mashindano ya Miss Tanzania yakifungiwa na BASATA mwaka jana, Kamati ya Miss Tanzania ikawa mpole, wala haijapimana ubavu na BASATA na kuanza kusukumiana lawama kupitia vyombo vya habari.
Kufungiwa kwa mashindano ya Miss Tanzania, kuliathiri vibarua vya zaidi ya watu 1000 ambao pengine kwa namna moja au nyingine, maisha yao na ya wanaowategemea yaliathirika kwa kiasi kikubwa.
Shilole anapobishana na BASATA na kuwasuta kwenye mahojiano yake kupitia mitandao ya kijamii, anapaswa kwanza ajiulize yeye na mashindano ya Miss Tanzania nani mkubwa?
Miss Tanzania ilikuwa na udhamini wa mamilioni kutoka kinywaji cha Redd’s kupitia Tanzania Breweries lakini BASATA haikujali hilo, sheria ikachukua mkondo wake …BASATA haikujali uhusiano wake mzuri na Tanzania Breweries ambayo inadhamini tuzo zake za Tanzania Music Awards kupitia Kilimanjaro Lager, ikatoa hukumu bila kupepesa macho.
Shilole inabidi ajiulize yeye ni nani mpaka apimane ubavu na chombo cha serikali, anategemea adhabu yake itasitishwa kwa njia hiyo? Je yuko juu ya sheria kiasi kwamba hastahili kuguswa? Anadhani BASATA wanafanya kazi kwa mashinikizo ya mitandao ya kijamii?
Nilipigwa na butwaa pale Shilole alipokuwa akiswashutumu BASATA kwa kusema:  “Mnataka nikaishi wapi? nina watoto wawili wanaosoma boarding, kila mwaka ninatakiwa nilipe milioni 5 kwa kila mmoja, nina watoto 3 yatima ninaowalea na kuwasomesha kupitia muziki huu huu ninaofanya ambao watu wengine, ninalipa kodi ya nyumba Milioni 7 kwa mwaka, mlitaka nikauze unga au niwe changudoa?”
Kwa maneno hayo ni wazi kuwa Shilole anapimana ubavu na BASATA, mbaya zaidi kuna wakati alikwenda mbali zaidi kwa kusema “Tutachukua hatua kwa hatua” …Nimwambie tu Shilole kuwa unapokuwa mkosaji halafu ukataka kupimana ubavu na serikali ni kitu flan amazing, sio amazing ile ya kuvutia kama wanavyoitumia watoto wa mjini, hapana ni amazing ya kuharibu – Inashangaza, inastaajabisha, inaduwaza!

SIMBA SC YA DYLAN KERR NI HATARI, MWINGINE ALA 3-0 LEO ZENJI...MAGURI 'AMEFUFUKA'

Elias Maguri akimiliki mpira mbele ya mabeki wa Jang'ombe Boys
ELIAS Maguri ameendelea kutesa kwa kuzifumania nyavu kisiwani Zanzibar, ambako klabu yake Simba SC imekuwa kambini ikicheza mechi za kujipima nguvu.
Jioni hii, Maguri amefunga bao moja Wekundu hao wakishinda 3-0 dhidi ya Jang’ombe Boys iliyopanda Ligi Kuu msimu ujao, katika uwanja wa Amaan.
Simba inayofundishwa na kocha Muingereza Dylan Kerr anayesaidiwa na mzalendo Selemani Matola, ilianza kuzihujumu nyavu za wapinzani wao katika dakika ya 14, Maguri akiwa ndiye mfungaji.
Dakika ya 17, Jang’ombe Boys wakamruhusu Michael Mgimwa kuandika bao la pili, na timu hizo zikaenda mapumziko Simba ikiongoza 2-0.
Simba ilihitimisha ushindi wao kwa bao la dakika ya 81 lililopachikwa kimiani na Samir Omar.
Huo ni mchezo wa nne kwa Simba SC kucheza na kushinda tangu ilipanza kambi yake kisiwani hapa mwanzoni mwa wiki iliyopita, awali ikiifunga kombaini ya Zanzibar 2-1, ikaitandika Black Sailors 4-0, Polisi 2-0 kabla leo kupata ushindi huo wa 3-0 dhidi ya Jang’ombe Boys.
Simba itakamilisha mechi zake Jumatano kwa kupambana na KMKM iliyotolewa hatua za makundi kwenye michuano ya kombe la Kagame iliyomalizika Jumapili, kabla ya kurejea Dar es Salaam Alhamisi. 

'MASISTA DUU' WAPENDA MAN U SASA HAWANA SABABU YA KUVAA MIJEZI YA KIUME

Klabu ya Manchester United imetoa jezi maalum za mashabiki wake wa kike .  PICHA ZAIDI GONGA HAPA

YANGA SC YAMUUZA SHERMAN MILIONI 300, ASAINI MIAKA MITATU MPUMALANGA BLACK ACESS

Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Mliberia Kpah Sean Sherman amesaini Mkataba wa miaka mitatu na klabu ya Mpumalanga Black Aces ‘AmaZayoni’ ya Afrika Kusini.
Habari za ndani zinasema Yanga SC italipwa dola za Kimarekani 150,000 (Sh. Milioni 300) kama ada ya uhamisho ya mchezaji huyo aliyesaini Jangwani kwa dola 60,000 (Sh. Milioni 120,000) Desemba mwaka jana.
Na Sherman aliyekuwa analipwa doka 3,000 (Sh. Milioni 6) kwa mwezi Yanga SC, sasa atakuwa analipwa dola 5,000 (Sh, Milioni 10) Black Aces kabla ya kukatwa kodi.
Kpah Sean Sherman baada ya kusaini Black Acess juzi

Mwenyekiti wa Aces, Mario Morfou ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE kwa simu leo kwamba wanatarajia Sherman atakuwa pacha mzuri wa Mzambia, Collins Mbesuma katika safu ya ushambuliaji ya timu yake msimu huu.
“Ni mchezaji mzuri na mmoja wa wachezaji bora sana tuliowahi kusaini na sasa tunajivunia kuwa naye AmaZayoni,” amesema Morfou.
Sherman alijiunga na Yanga SCS Desemba mwaka jana akitokea klabu ya Cetinkaya ya Ligi Kuu ya Cyprus Kaskazini na katika kipindi hicho ameichezea timu ya Jangwani mechi 27 na kuifungia mabao sita kwenye mashindano yote.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miak 23 sasa, alianza kuichezea Cetinkaya mwaka 2012, akitokea Duzkaya SK aliyoanza kuichezea mwaka 
2010, akitokea Barrack YC ya nyumbani kwao, Liberia ambayo alianza kuichezea mwaka 2009.

ONYESHO LA TWANGA PEPETA JANA TCC CLUB

Mwimbaji wa bendi ya Africans Stars 'Twanga Pepeta' Ige Moyaba akiimba katika onyesho la bendi hiyo jana ukumbi wa Sigara (TCC), Chang'ombe, Dar es Salaam usiku wa jana 

Waimbaji wa Twanga wakiimba jana

Mpiga gitaa la solo maarufu, Adolph Mbinga akifanya yake jana

Wakubwa wakipata burudani jana

Wanachama wa CCM baada ya kupiga kura za Madiwani na Wabunge wa chama chao jana, walijimwaga TCC

Hizi ni hisia au? Juma Mbizo jana hakuwa na furaha kabisa

Enock Bwigane naye alikuwepo jana TCC

Hassan Moshi naye alikuwepo jana TCC

Zai Simba (kulia) na shoga yake Joan walikuwepo TCC

Le Mutuz alikuwepo na kimwana huyu jana TCC

ARSENAL WAIKALISHA CHELSEA MECHI YA NGAO 1-0 WEMBLEY

Wachezaji wa Arsenal wakisherehekea ushindi wao wa Ngao ya Jamii leo baada ya kuifunga Chelsea 1-0 PICHA ZAIDI GONGA HAPA

KOCHA Mfaransa Arsene Wenger amevunja ‘uteja’ wake kwa Mreno, Jose Mourinho leo. Wenger ameshinda mechi ya kwanza dhidi ya Mourinho katika mechi 14, baada ya kuiwezesha Arsenal kutwaa Ngao ya Jamii England kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Chelsea Uwanja wa Wembley, London.
Hilo ni taji la pili ndani ya miezi mitatu kwa Arsenal, baada ya miezi miwili na ushei iliyopita kutwaa Kombe la FA katika fainali iliyopigwa uwanja huo huo.
Kipa wa zamani wa Chelsea, Petr Cech alidaka kwa ustadi mkubwa huku bao pekee la Arsenal likifungwa na kiungo Alex Oxlade-Chamberlain dakika ya 24.
Kikosi cha Arsenal kilikuwa; Cech, Bellerin, Mertesacker, Koscielny, Monreal, Coquelin, Ramsey, Oxlade-Chamberlain/Arteta dk77, Cazorla, Ozil/Gibbs dk82 na Walcott/Giroud dk66.
Chelsea: Courtois, Ivanovic, Cahill, Terry/Moses dk82, Azpilicueta/Zouma dk69, Matic, Ramires/Oscar dk54, Willian, Fabregas, Hazard na Remy/Falcao dk45. 

AZAM FC WALIVYOKABIDHIWA 'MLIMBWENDE' WA KAGAME BAADA YA KUIKALISHA GOR MAHIA TAIFA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidy Meckysadick (wa pili kushoto) akimkabidhi la ubingwa wa soka Afrika Mashariki na Kati, Kagame baada ya kuifunga Gor Mahia ya Kenya 2-0 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Bocco akikabidhiwa donge la dola za KImarekani 30,000 kwa ubingwa wa Kagame

Wachezaji wakifurahia baada ya mechi leo

AZAM FC BINGWA KOMBE LA KAGAME 2015, GOR MAHIA WAFA 2-0 TAIFA

Nahodha wa Azam FC, John Raphael Bocco akishangilia baada ya kuifungia Azam FC bao la kwanza katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Gor Mahia leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
AZAM FC wametwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuifunga mabao 2-0 Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa fainali uliofanyia Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
Azam FC wanakuwa timu ya kwanza ya Tanzania nje ya Simba na Yanga SC kutwaa taji hilo- wakishiriki kwa mara ya tatu tu mashindano hayo baada ya mwaka 2012 walipofika fainali na kufungwa na Yanga SC 2-0 Dar es Salaam na mwaka jana kutolewa kwa penalti 4-3 mjini Kigali, Rwanda baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90 katika Robo Fainali na El Merreikh ya Sudan walioibuka mabingwa.
Timu hiyo yenye maskani yake Azam Complex, Chamazi, Mbade, Temeke mjini Dar es Salaam imeshinda mechi zake zote kuanzia Kundi C bila kuruhusu nyavu zake kuguswa hata mara moja- na ‘ilipata shida’ kidogo tu mbele ya Yanga SC katika Robo Fainali ilipolazimika kushinda kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 0-0 dakika 90, wakati Nusu Fainali iliilaza KCCA 1-0. 

Kikosi cha Azam FC kilichoanza leo; Waliosimama kutoka kulia ni John Bocco, Shomary Kapombe, Serge Wawa Pascal, Aggrey Morris, Ame Ali 'Zungu' na Jean Baptiste Mugiraneza. Walioinama kutoka kulia ni Said Mourad, Himid Mao, Aishi Manula, Farid Mussa na Kipre Herman Tchetche 
Kwa ushindi huo, timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake inazawadiwa kitita cha dola za Kimarekani 30,000 (Sh. Milioni 60), wakati Gor Mahia wanapozwa na dola 20,000 (Sh. Miliioni 40).
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Louis Hakizimana wa Rwanda aliyesaidiwa na Nagi Ahmed wa Sudan na Suleiman Bashir wa Somalia, hadi mapumziko tayari Azam FC walikuwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Bao hilo lilipatikana dakika ya 16, mfungaji Nahodha John Raphael Bocco ‘Adebayor’ aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Kipre Herman Tchetche kutoka upande wa kulia.
Azam FC walitawala mchezo vizuri kwa dakika 20 za mwanzo, lakini baada ya hapo kasi yao ikapunguzwa na uchezaji wa rafu wa wachezaji wa Gor Mahia ambao hawakuchukuliwa hatua yoyote na refa Hakizimana. 
Wachezaji wa Gor walikuwa wakiwapiga viwiko na mateke wachezaji wa Azam FC na kuanguka chini wakitokwa hadi damu, lakini hiyo haikumfanya refa Hakizimana japo kutoa kadi ya njano.
Hali hiyo iliwafanya washambuliaji wa Azam waanze kucheza kwa woga na kupunguza kasi yao ya mashambulizi- huku Gor Mahia wakitumia mwanya huo nao kuanza kushambulia.
Medie Kagere alikaribia kuisawazishia Gor Mahia dakika ya 22 kama si beki muhimili wa ukuta wa Azam FC, Serge Wawa Pasacal kuokoa.
Kipindi cha pili, kocha Stewart Hall wa Azam FC alianza na mabadiliko akimtoa winga Farid Mussa Malik na kumuingiza beki David Mwantika.
Mabadiliko hayo yaliyolenga kuimarisha ulinzi yaliisaidia Azam FC kupunguza kasi ya Gor Mahia na kufanikiwa kuendelea kutawala mchezo. 
Mshambuliaji nyota kutoka Ivory Coast, Kipre Herman Tchetche akaifungia bao la pili Azam FC dakika ya 64 kwa shuti la mpira wa adhabu lililompita kama mshale kipa wa Gor Mahia, Boniphace Olouch.
Mfungaji wa bao la pili la Azam FC, Kipre Herman Tchetche akimtoka beki wa Gor Mahia
Mshambuliaji aliyechezeshwa nafasi ya kiungo leo, Ame Ali 'Zungu' kulia akizuia shuti la beki wa Gor Mahia, Harun Shakava
Winga machachari wa Azam FC, Farid Mussa Malik akiruka na mpira wake kwanja la beki wa Gor Mahia, Harun Shakava   

Faulo hiyo ilitokana na beki Harun Shakava kumuangusha beki wa Azam FC, Shomary Kapombe nje kidogo ya boksi.
Mchezo uliotangulia mchana wa leo, KCCA ya Uganda iliifunga 2-1 Khartoum N ya Sudan na kumaliza katika nafasi ya tatu.
Kikosi cha Azam FC kilikuwa; Aishi Manula, Aggrey Morris, Morald Said, Pascal Wawa, Farid Mussa/Erasto Nyoni dk46, Shomari Kapombe, Jean Mugiraneza, Himid Mao, Ame Ali/Frank Domayo dk69, John Bocco na Kipre Tchetche/dk88.
Gor Mahia; Boniphace Olouch, Mussa Mohammed, Sibomana Abouba, Harun Shakava, Karim Nzigiyimana, Innocent Wafula/Enock Agwanda dk83, Khakid Aucho, Godfrey Walusimbi, Medie Kagere/George Odhiambo dk83, Michael Olunga na Erick Ochieng/Ali Abondo dk74. 

KCCA WASHINDI WA TATU KAGAME, WAITANDIKA 2-1 KHARTOUM N TAIFA, WAONDOKA MILIONI 20

KCCA ya Uganda imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame baada ya kuifunga mabao 2-1 Khartoum N ya Sudan.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya KCCA yamefungwa na Muzamiru Mutyaba na Michael Birungi, wakati bao pekee la Khartoum N limefungwa na Osmaila Baba.
Na kwa ushindi huo, KCCA itapata zawadi ya fedha, dola za Kimarekani 10,000 (Sh. Milioni 20 za Tanzania) wakati Khartoum inaondoka mikono mitupu sawa na timu nyingine zilizotolewa awali.
Fainali ya michuano hiyo inafuatia Saa10:00 kati ya Gor Mahia ya Kenya na Azam FC ya Tanzania na bingwa ataaawadiwa dola 30,000 (Sh. Milioni 60) mshindi wa pili dola 20,000 (Sh. Milioni 40).

SIMBA SC WACHARUKA, WASAJILI STRAIKA LA DC MOTEMA PEMBE

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
ZIKIWA zimebaki siku nne kabla ya dirisha la usajili la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kufungwe, Simba SC Simba imemsajili mshambuliaji wa DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Danny Lyanga (pichani). 
BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE inafahamu Simba SC ilimalizana na mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union ya Tanga juzi.
Lyanga amesaini mkataba wa miaka miwili na leo anatarajiwa kuelekea Zanzibar kuungana na wachezaji wengine walioko huko wakijinoa chini ya Kocha Mkuu Muingereza, Dylan Kerr.
Kusajiliwa kwa Lyanga na kutapoza machungu ya Simba SC kumkosa mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo, ambaye licha ya kumalizana na Wana Msimbazi, lakini klabu yake ikataka 'dau la rekodi' kumuachia.
Ndani ya siku tatu Simba SC inakuwa sasa imesajili wachezaji wapya watatu, wengine wakiwa ni kiungo Mzimbabwe, Justice Majabvi na beki Mrundi, Emery Nimubona. 

MANCHESTER CITY YAFUMULIWA 4-2 UJERUMANI

Mshambuliaji wa Manchester City, Raheem Sterling akimtoka beki wa Stuttgart ya katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Mercedes Benz Arena mjini Stuttgart, Ujerumani jana. Wenyeji walishinda 4-2, mabao yao yakifungwa na Daniel Ginczek mawili, Filip Kostic na Daniel Didavi wakati ya City yalifungwa na Kelechi Iheanacho na Edin Dzeko  PICHA ZAIDI GONGA HAPA

LUKE CAMPBELL AMTWANGA 'KAMA BEGI' TOMMY COYLE PAMBANO LA WBC

Luke Campbell akiinua mikono juu kushangilia baada ya kumbwaga chini mpinzani wake, Tommy Coyle raundi ya pili usiku wa jana katika pambano la kuwania kugombea ubingwa wa WBC uzito wa Light. Luke Campbell alimshinda Tommy Coyle kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya Uwanja wa KC. PICHA ZAIDI GONGA HAPA

ORIGI, COUTINHO WOTE WAFUNGA LIVERPOOL IKISHINDA 2-0 HELSINKI

Mshambuliaji mpya wa Liverpool, Divock Origi akishangilia baada ya kuifungia timu yake jana katika ushindi wa 2-0 dhidi ya wenyeji HJK Helsinki mchezo wa kirafiki. Bao lingine la Liverpool lilifungwa na Philippe Coutinho. PICHA ZAIDI GONGA HAPA

KIPA WA CHELSEA AANZA VYEMA SIMBA SC, ADAKA ‘KINOMA’, MNYAMA AUA 2-0 ZENJI

Angban wa pili kulia walioinama akiwa katika kikosi cha Simba SC jana
KIPA aliye katika majaribio Simba SC, Vincent Angban kutoka Ivory Coast jana ameanza vizuri baada ya kuidakia timu hiyo ikishinda 2-0 dhidi ya Polisi Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Mabao ya Simba SC jana yamefungwa na Mussa Hassan Mgosi kipindi cha kwanza na Elius Maguli kipindi cha pili.
Angban aliyewahi kudakia timu ya vijana chini ya umri wa miaka 21 ya Chelsea ya England, alianzia Azam FC, lakini hakukubalika mbele ya kocha Muingereza Stewart Hall akaomba kujaribu bahati yake na Simba SC.
Na kocha Muingereza wa Simba SC, Dylan Kerr akamuanzisha jana katika mchezo wa kirafiki na kudaka vizuri, timu ikishinda kwa mara ya tatu mfululizo mechi za kirafiki visiwani humo. 
Awali Simba SC iliifunga Kombaini ya Zanzibar 2-1 kabla ya kuifunga 4-0 Black Sailor hapo hapo Uwana wa Amaan na kesho watacheza na Jang’ombe Boys kabla ya Jumatano KMKM Saa 10:00 jioni. 
Hamisi Kiiza akiwania mpira dhidi ya kipa wa Polisi
Mussa Mgosi akipambana na beki wa Polisi

CECAFA ACHENI KIBURI, YARUDISHENI MASHINDANO JANUARI, HAYANA FAIDA

HATIMAYE bingwa mpya wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame anatarajiwa kupatikana jioni ya leo kwa mchezo wa fainali kati ya wenyeji Azam FC na Gor Gor Mahia ya Kenya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo utatanguliwa na mechi ya kusaka mshindi wa tatu kati ya KCCA ya Uganda na Khartoum N ya Sudan, itakayoanza Saa 8:00 mchana.
Imeshuhudiwa katika michuano ya mwaka huu, mabingwa watetezi, El Merreikh ya Sudan wakishindwa kuja kwa sababu wapo katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Na hata washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Sudan, El Hilal nao hawakuja kwa sababu wapo kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika- badala yake ndio wamekuja washindi wa tatu na wa nne, Al Shandy na Khartoum.
Hakuna ubishi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, klabu hizo mbili za Sudan zipo juu zaidi kisoka na hata kwa uwezo wa kujiendesha, tena kisasa kabisa.
Kwa miaka ya karibuni imekuwa kawaida kwa timu stahiki kutojitokeza katika Kombe la Kagame kutokana na sababu za kawaida sana.
Kwa mfano mwaka jana, Yanga SC walitakiwa kusafiri hadi Rwanda, lakini wakagoma kwa sababu ndiyo kwanza walikuwa wanaanza maandalizi ya msimu mpya.
Miaka ya nyuma, mashindano haya wakati huo yakijulikana kama Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati tu hakuna timu iliyostahili ilikuwa inakosekana.
Mashindano haya wakati huo yalikuwa yafanyika Januari ya kila mwaka na yalikuwa yanafana mno.
Timu nyingi zilichangamkia fursa ya kushiriki michuano hiyo, kwa sababu baada ya hapo zilikuwa zinaingia moja kwa moja kwenye michuano mikubwa ya Afrika- Kombe la Washindi, Kombe la CAF na Klabu Bingwa Afrika.
Kwa sasa Kombe la CAF limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho ndiyo hilo limefanya tuwakose El Hilal na Klabu Bingwa sasa imekuwa Ligi ya Mabingwa, ambayo nayo imefanya tuwakose Merreikh.
Michuano hii ilianza taratibu kutoka katika muda wake mwafaka wa kufanyika, kutokana tu na sababu za ukosefu wa fedha za maandalizi.
Ilisogezwa mbele kidogo kidogo hadi sasa kalenda yake imekuwa Julai na Agosti.
Julai na Agosti ni kipindi ambacho michuano ya CAF inafikia kwenye hatua ya makundi- lakini kwa sababu Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limejikatia tamaa, halioni umuhimu tena wa michuano hiyo ya bara zima.
Sasa ni dhahiri sisi wa CECAFA ndiyo tunashika mkia kisoka katika bara letu, hata nchi ndogo ndogo zilizokuwa duni kisoka miaka michache iliyopita kama Madagascar, Lesotho, Swaziland na Shelisheli za kusini (COSAFA) sasa zinatufundisha mengi. 
Hii ni kwa sababu, pamoja na mapungufu yetu yote, lakini pia hatuna mipango.
Mfano mdogo ni hii michuano ya Kagame, badala ya kuifanya Januari ili timu zetu zipate maandalizi ya kuingia kwenye michuano ya Afrika, tunaifanya Julai na Agosti.
Kipindi hicho ni ambacho baadhi ya Ligi za ukanda wetu zinatoka kumalizika na ligi nyingine zinaelekea kuanza, unaweza kuona kabisa timu nyingi huingia katika mashindano haya zikiwa haziko tayari.
Mashindano haya yakirudi kufanyika Januari, dhahiri yatarejesha msisimko wake na hakutakuwa na udhuru wa timu kutokuja kushiriki.
Hata ile dhamira ya kualika timu kubwa za ukanda mwingine kuja kutongezea changamoto inaweza kufanikiwa kwa sababu hicho ni kipindi ambacho hakuna mashindano ya CAF.
Lazima turejeshe enzi zile bingwa mtetezi anapokewa kwenye kituo cha mashindano akiwa na Kombe lake. Turejeshe enzi ambazo mashindano yanashirikisha mabingwa watupu wa ukanda wetu.
Turejeshe thamani ya mashindano kwamba si ya kila timu kushiriki, yawe mashindano ya mabingwa wa ukanda wetu.
Novemba na Desemba tunafanya Challenge (Kombe la Mataifa ya CECAFA), Januari mapema tu ndani ya wiki mbili za mwanzo tunakamilisha Kagame- baada ya hapo, klabu zetu ziende kwenye michuano ya Afrika zikiwa vizuri.
Lakini ajabu CECAFA wameshindwa kuelewa dhana hii na wameendelea kulazimisha Kombe la Kagame lifanyike Julai na Agosti, ndiyo maana watu sasa wanayaita mashindano haya Bonanza tu, kwa sababu hawaoni umuhimu wake.
Wakati umefika sasa viongozi wa CECAFA wakubali kushaurika na mashindano wayarudishe Januari. Tukutane Taifa. 

SIMBA SC YAMPIGA CHINI MAVUGO, YAMSAJILI NIMUBONA, AWASILI LEO DAR MOJA KWA MOJA ZENJI

Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
SIMBA SC imeamua kuachana na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo (pichani) baada ya klabu mbili za nchini humo kuopandisha thamani ya mchezaji huyo na kuwa Sh. Milioni 200, badala 110 zilizokubakiwa awali.
Rais wa Simba SC, Evans Elieza Aveva ameiambia BIN ZUBEIRY SPORTS- ONLINE leo kwamba, pamoja na jitihada za kutuma biongozi Bujumbura kwa mijadala mirefu suala hilo limeshindikana na sasa wanaelekeza nguvu zao katika kusaka mchezaji mwingine. 
“Wakati mchakato huu ukiendelea Simba SC ilikuwa inaendelea na mazungumzo na washambuliaji kadhaa wa kimataifa Ili kuwa na wigo mpana wa kuchagua. Tunaamini tutasajili mchezaji mzuri na bora ambaye thamani na uwezo wake utashabihiana au kuwa zaidi,”amesema Aveva.
Aveva amesema walikubaliana mchezaji asajiliwe kwa Sh 110 milioni baada ya michuano ya Ligi Kuu na Kombe la FA Burundi na Simba SC ilimtuma Makamu wake wa Rais, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ aende Bujumbura kukamilisha majadiliano na uongozi wa Vital’O juu ya usajili wa Laudit Mavugo. 
Lakini ajabu, Vital’O wakabadilika na kuongeza maradufu thamani ya mchezaji huyo pamoja na vipengele vipya vya mauzo kinyume na makubaliano ya awali.
“Thamani mpya ya mchezaji imepandishwa na kuwa Tshs 200 milioni kutoka ile ya awali ya Tsh 110 milioni ambazo zilijumuisha gharama za kumlipa mchezaji.”amesema Aveva.
Aidha, kumeibuka pia mzozo mpya kati ya klabu ya Vital’O FC na Solidarity FC, inayodai kumlea Mavugo, hivyo nayo kudai ina hakimiliki ya mchezaji huyo.
“Licha ya mkanganyiko wa umiliki wake, Vital’O imedai kuwepo kipengele kipya kinachodai mapato ya asilimia 50 kama mchezaji huyo atauzwa na Simba SC kwenda klabu nyingine,”amesema.
Lakini pamoja na hayo, Aveva amesema Simba SC imefarijika kwa kumpata beki wa kimataifa wa Burundi kutoka klabu ya Vital’O, Emery Nimubona ambaye atawasili nchini leo na moja kwa moja kwenda kujiunga na timu kambini Zanzibar.
Beki huyo wa zamani wa Athletico Olympic ya Burundi pia, anacheza beki zote mbili, kulia na kushoto.

WOLFSBURG WAIDUNDA BAYERN MUNICH MECHI YA SUPER CUP UJERUMANI

Wachezaji wa Wolfsburg wakisherehekea ushindi wa taji la Super la Ujerumani baada ya kuifunga Bayern Munich kwa penalti 5-4 kufuatia sare ya 1-1, bao la Bayern likifungwa na Arjen Robben na Wolfsburg wakisawazisha kupitia kwa Nicklas Bendtner. Penalti za washindi zilifungwa na Rodriguez, De Bruyne, Schurrle, Kruse na Bendtner wakati za BayernSCORED - Vidal, Bayern zilifungwa na Alonso, Robben, Lahm na Costa huku Alonso akikosa. PICHA ZAIDI GONGA HAPA

HOMA YA MECHI NA TAIFA STARS, MALAWI WAMTEUA MTAWALI KOCHA MPYA

NYOTA wa zamani wa klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, Ernest Mtawali (pichani) amechaguliwa kuwa kocha wa timu ya taifa ya Malawi, 'The Flames'.
Uteuzi huo unakuja siku chache baada ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kutoa ratiba ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia 2018, Malawi ikipangwa kuanza na Tanzania, Taifa Stars katika mchujo wa awali.
Mtawali amepewa Mkataba wa mwaka mmoja akirithi mikoba ya mchezaji mwingine wa zamani wa kimataifa wa Malawi, Young Chimodzi aliyefukuzwa Juni mwaka huu baada ya The Flames kufungwa nyumbani 2-1 na Zimbabwe katika mechi ya Kundi L kufuzu Fainali za Mataiofa Afrika mwaka 2017.
Rais wa Chama cha Soka Malawi, Walter Nyamilandu amemtambulisha Mtawali sambamba na Msaidizi wake, Nsanzuwrimo Ramadhan katika Kituo cha Ufundi na Maendeleo cha Chiwembe mjini Blantyre leo asubuhi.
Nyamilandu amewaambia Waandishi wa Habari kwamba Mtawali amepewa jukumu la kuhakikisha The Flames inafanya vizuri katika mechi za kufuzu AFCON 2017 pamoja na Kombe la Dunia 2018 na Mtawali amefurahia changamoto hiyo mpya.

AZAM FC NA GOR MAHIA FAINALI KOMBE LA KAGAME KIINGILIO BUKU TATU TU

Na Baraka Kizuguto, DAR ES SALAAM
MICHUANO ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inatarajiwa kufika tamati kesho jumapili katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kwa mchezo wa Fainali utakaozikutanisha timu ya Azam FC dhidi ya Gor Mahia.
Viingilio vingine vya mchezo huo wa kesho wa fainali ke ni VIP A ni shilingi elfu kuni na tano (15,000) na VIP B & C, Shilingi elfu kumi (10,000) na sehemu nyingine ya uwanja  iliyobakia ni shilingi elfu tatu (3,000) kwa viti vya rangi ya bluu, kijani na rangi ya chungwa.
Katika mchezo wa nusu fainali uliofanyika jana, Gor Mahia iliweza kuibuka na ushindi wa mabao 3- 1 dhidi ya Khartoum mabao yaliyofungwa na Michael Olunga, Innocent Wafula na Kagere Meddie na kukata tiketi ya kucheza fainali.
Kila la heri Azam FC kesho mbele ya Gor Mahia

Gor Mahia chini ya kocha wake Frank Nuttal mpaka kufikia hatua ya fainali, imecheza jumla ya michezo sita, ikiwemo michezo minne katika hatua ya makundi, robo fainali na nusu fainali, ambapo imeweza kushinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja.
Mshambuliaji wa Gor Mahia,Michael Olunga anaongoza kwa ufungaji, akiwa amepachika mabao matano, akifuatiwa na nahodha wa Khartoum Salehdin Osman na msadizi wake Amin Ibrahim wote wenye mabao manne kila mmoja.
Kwa uapnde wa Azam chini ya kocha wake Stewart Hall, imefanikiwa kufika hatua ya fainali bila ya kuruhusu nyavu zake kutikisika, huku safu yake ya ushambuliaji ikiwa imepachika mabao tisa (9) katika michezo mitano iliyocheza kuanzia hatua ya makundi.
Kuelekea mchezo wa Fainali, Azam FC iliziondosha Yanga SC kwa mikwaju ya penati (5-4) hatua ya robo fainali, na kasha kuindoa KCCA hatua ya nusu fainali kwa kuifunga kwa bao 1- 0, bao lililofungwa na mshambuliaji chipukizi Farid Musa.
Mshambuliaji Kipre Tchetche ana mabao matatu kwa upande wa washambuliaji wa Azam FC, akifuatiwa na nahodha John Bocco na Farid Musa wenye mabao mawili kila mmoja.
Katika fainali hiyo ya kesho, inatarajiwa kuwa ya vuta ni kuvute kutokana na makocha wa timu hizo, Frank Nuttal wa Gor Mahia kutaka kushinda taji hilo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30 tangu Gor Mahia kushinda kombe hilo mara ya mwisho mwaka 1985 walipotwaa kwa mara ya tano (5).
Huku Stewart Hall akiwania kuweka historia ya kwanza kwa klabu ya Azam FC kuweza kutwaa kombe hilo kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo miaka tisa iliyopita, baada ya kusindwa kutwaa taji hilo ilipotinga fainali mwaka 2012 kwa kufungwa na Yanga SC mabao 2-0.
Mchezo huo wa fainali unatarajiwa kuanza saa 9:45  alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, huku mchezo wa kusaka mshindi wa tatu ukitarajiwa kuanza saa 7:30 mchana ukizikutanisha timu za Khartoum ya Sudan dhidi ya KCCA kutoka nchini Uganda.
Bingwa wa michuano hiyo atazawadiwa kitita cha Dola za Kimarekani Elfu Thelathini (U$ 30,000), mshindi wa pili Dola za Kimarekani Elfu Ishirini (U$ 20,000) huku mshindi wa tatu akizawadiwa Dola za Kimarekani Elfu Kumi (U$ 10,000).
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi nchini Mkoa wa Temeke, linawashikilia watu watatu  kutoka nchini Kenya kufuatia kufanya kosa la shambulio katika mchezo wa nusu wa fainali kati ya Gor Mahia dhidi ya Khartoum katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Raia hao wa Kenya walifanya shambulio kwa mlinzi wa TFF uwanja wa Taifa, Omary Mayai wakiwa katika jukwaa la VIP A ambapo askari polisi walijaribu kuwaonya na kuwaomba kuwa wastaarabu, lakini walishidwa kutii amri ya polisi na kuendelea kufanya vurugu kabla ya mmoja wao kukimbilia ndani ya uwanja na kuketi katika benchi la ufundi la Gor Mahia.
Namba ya jarada la kesi iliyofunguliwa kituo cha Polisi cha Chang’ombe ni CHA/RB6265/2015, na wanaoshikiliwa kituoni hapo ni mshabiki wa Gor Mahia Jackson Mjidie (Jaro Soja), pamoja na waandishi wa habari wawili kutoka kituo cha Citizen, Okinyi Mike na Jariri Otieno.

Top