Fabrice Muamba "ameweza kuwatambua jamaa zake na kujibu
maswali kwa usahihi", taarifa iliyotolewa kwa pamoja na klabu yake ya
Bolton na hospitali ilieleza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 ameweza "kupumua
bila kutegemea mashine" lakini bado ameendelea kubakia katika chumba cha
wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa hali ya juu baada ya kuanguka na kuzirai
kutokana na matatizo ya moyo siku ya Jumamosi.
Taarifa ya pamoja iliyotolewa na hospitali ya London Chest na
Bolton ilisema anaendelea "kuonesha maendelea mazuri ya afya yake".
Taarifa hiyo imeongeza hali yake haikuwa mahututi lakini
ameendelea kuwa mgonjwa sana.
Taarifa iliyotolewa mapema ilisema "anaweza pia
kuchezesha mikono na miguu yake" lakini "hali yake kwa siku za baadae
haitafahamika kwa muda fulani".
Mchezaji huyo wa zamani wa timu ya taifa ya England chini ya
umri wa miaka 21, amekuwa katika hospitali hiyo ya maradhi ya moyo tangu siku
ya Jumamosi wakati wa mechi ya kuwania Kombe la FA hatua ya robo fainali katika
uwanja wa White Hart Lane.
Mchumba wake, Shauna Magunda, ambaye ni mama wa mtoto wake
mmoja wa kiume aitwae Joshua, alituma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa
Twitter siku ya Jumatatu jioni akisema: "Sala zenu zote zinafanya kazi
nawashuru wote kwa dhati. Kila sala imemfanya aimarike zaidi."
Muamba alizaliwa Zaire, sasa inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Congo na alifika England na umri wa miaka 11 akiwa mkimbizi.
Rais wa Chama cha kabumbu cha DRC Omari Selemani alisema
kiungo huyo anaungwa mkono na watu "milioni 65" wa Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo.
Siku za nyuma mchezaji huyo alikataa jaribio la chama cha
kabumbu cha Congo walipomuita aichezee timu ya taifa na badala yake akachagua
kuichezea timu ya vijana ya England.



.png)
0 comments:
Post a Comment