• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 28, 2012

  TOFAUTI YA PAPIC WENU NA MILOVAN WAO...

  Papic, kocha wa Yanga
  JUMAPILI Simba SC, ilianza vyema Raundi ya Pili ya Kombe la Shirikisola Soka Afrika, baada ya kuilaza ES Setif ya Algeria mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Kwa matokeo hayo, Setif ina kazi ngumu kwenye mchezo wa marudiano wiki mbili baadaye Uwanja wa nyasi bandia, Mei 8, mjini Stif uliofunguliwa mwaka 1972 na kukarabatiwa mwaka 2008, ukiwa na uwezo wa kumeza watu 25,000 tu, kwani itatakiwa kushinda 3-0 ili isonge mbele.
  Ikishinda 2-0, mchezo utarefushwa hadi dakika 120 ambazo zitafanya jumla ya dakika 210 na wasipofungana pia hapo, mikwaju ya penalti itabeba jukumu la kuamua timu ya kusonga mbele.
  Katika mchezo wa Jumapili, Simba ilionyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, ingawa kweli wapinzani hawakuwa sumu sana, lakini inaweza kuwa ilichangiwa na uchezaji mzuri wa Wekundu wa Msimbazi siku hiyo.
  Kipindi cha kwanza, kidogo hakikuwa na mwelekeo mzuri, ingawa mara nyingi soka ndio huwa hivyo.
  Hakukuwa na uelewano mzuri sana kati ya viungo na washambuliaji na matokeo yake kazi bure zilikuwa nyingi sana, lakini kipindi cha pili Simba walibadilika mno na pengine hiyo ilitokana na maelekezo waliyopewa wakati wa mapumziko.
  Tuliishuhudia Simba ikicheza kwa kasi ile ile mwanzo hadi mwisho wa mchezo na huwezi kusema wachezaji waliotokea benchi waliongeza nguvu, hapana kwani waliingia dakika zimekwishayoyoma mno.
  Sifa zimuendee kocha wa Simba, Mserbia Profesa Milovan Cirkovic ambaye alifanya kazi nzuri ya kuwandaa vijana wake hata wakaleta matokeo hayo mazuri.
  Ilishuhudiwa katika mazoezi ya timu hiyo kabla ya mechi na Setif, Milovan akifanya kazi ya kuiandaa timu kwa utulivu, umakini na weledi wa hali ya juu.
  Aliifanyia kazi idara moja baada ya nyingine na waandishi wa habari walipokuwa wakienda walikuwa wakiripoti kazi nzuri ya kocha huyo, asiye na munkari.
  Mwezi uliopita tu Simba ilikuwa mbovu na hata kufuzu kwake kutoka Raundi ya Kwanza, wakiitoa Kiyovu Sport ya Rwanda kulikuwa kwa bahati tu, lakini sasa hali imebadilika.
  Kwa nini? Jibu ni Milovan.
  Huyu ni kocha Mserbia kama wa Yanga, Kostadin Bozidar Papic, lakini wana tofauti kubwa katika utendaji wa kazi.
  Kwanza Milovan hashobokei magazeti. Siyo kocha wa magazeti anaandikwa magazetini kwa sababu maalum haandikwi ovyo ovyo kama Papic, hadi maisha yake binfasi. Hata akiibiwa taulo chumbani kwake, kesho yake utasoma kwenye magazeti, tena yeye mwenyewe akiwa chanzo cha habari.
  Milovan ametulia anajua nini kilichomleta Tanzania na hapana shaka kwa kutambua kabisa makocha wote hawana bahati kama ya Arsene Wenger au Alex Ferguson, anataka hata siku yakimkuta kama yaliyomkuta Claudio Ranieri Inter Milan juzi, basi awe ameacha kitu cha kumfanya akumbukwe daima Simba SC.
  Wakati Simba inacheza ovyo, Milovan alikuwa akilaumiwa naye hata siku moja hakuwahi kutoa visingizio, zaidi ya kuendelea na programu yake hatimaye leo wana Simba wanafurahia timu yao kwa matokeo na mchezo mzuri.
  Unaweza kuona namna anavyoiunda Simba upya, au anavyoiboresha timu kwa kuinua vipaji vya wachezaji makinda kama Ramadhan Singano ‘Messi’ na Gerald Mkude- jinsi anavyotengeneza mfumo mzuri wa uchezaji kwa timu kushambulia zaidi.
  Namna anavyoweza kuwatumia washambuliaji wake wote hatari Haruna Moshi ‘Boban’, Felix Sunzu na Emanuel Okwi kwa wakati mmoja, tena wakati huo huo akiwa na kiungo mwingine wa pembeni mwenye kasi, Salum Machaku.
  Milovan anafanya kazi na ineonekana. Vipi Mserbia wa Yanga, Papic?
  Wiki iliyopita alikaririwa akisema washambuliaji Kenneth Asamoah na Davies Mwape hawana makali.
  Hawa ni wachezaji ambao aliwasajili yeye mwenyewe katika klabu ya Yanga. Viongozi wa Yanga walikuwa hawawajui hawa kama si yeye kuwakingia kifua wasajiliwe.
  Lakini ni kweli hawa wachezaji hawana makali, au kocha ndiyo kakosa mipango ya kuwatengeneza? Hilo ni swali ambalo nataka nishirikiane na wasomaji wangu kwa kurejea uchezaji wa wachezaji hao awali.
  Wakati mwingine hata mfumo wa kocha unamfanya mchezaji awe na makali au apooze na ndiyo maana hivi sasa, Hamisi Kiiza analalamika nafasi anayopangwa na kocha wake ya winga.
  Huyu ndiye Papic ambaye mara tu baada ya kurejea Yanga, alianza vita na kiungo aliyetoa krosi ya bao pekee la ushindi katika fainali ya Kombe la Kagame, Julai mwaka jana- klabu hiyo ikitwaa taji hilo tangu ilipotwaa mara ya mwisho mwaka 1993.
  Lakini ilikuwaje mzunguko wa pili winga Julius Mrope akaondolewa kwenye kikosi cha Yanga wakati mchezaji huyu alikuwa yuko vizuri hadi kufikiriwa kurithi mikoba ya Mrisho Ngassa?   
  Papic ni kocha mlalamishi mno- na mara kwa mara amekuwa akitishia kuacha kazi, wakati kurejea kwake Yanga, kulitokana na jitihada zake mweyewe. Haridhishwi na mazingira ya kazi, kwa nini anaendelea kufanya?
  Sitaki aondoke, nataka abadilike sasa, awe kama Mserbia mwenzake, ambaye yeye kazi yake ndio inayompatia umaarufu na si kuzungumza sana na magazeti.
  Papic, kama wasifu wake unavyosema ni kocha mwenye uzoefu na amefundisha klabu kubwa Afrika- kwanza anatakiwa kutofautisha klabu alizofundisha huko na Yanga na baada ya hapo akubaliane na Jangwani na mazingira yake.
  Hakuna anayeweza kukataa Yanga ina matatizo. Tena makubwa, kuanzia mfumo na uongozi kwa ujumla na hayo hayawezi kuisha mara moja, itachukua muda, lakini pia hayawezi kumzuia kocha kufanya kazi yake.
  Hao Simba wenyewe wana matatizo, lakini hayavumi kwa sababu Milovan amekubaliana nayo. Simba wapo kama timu. Kitu kimoja. Maumivu yao wote, furaha yao wote. Lakini Yanga kuna watu ambao wanependa kujitoa kwenye matatizo na kutaka watajwe katika mafanikio tu.
  Hicho kitu hakuna dunia nzima ni sawa na kufikiria kwenda peponi kabla ya kufa. Jose Mourinho sasa hivi anaelekea kutwaa mataji mawili kwa mpigo Real Madrid, Ligi ya Mabingwa na La Liga, lakini amepitia katika mwanzo mgumu sana Hispania ikiwemo kunyanyaswa na Barca katika El Classico.
  Papic afanye kazi. Aache mambo yake mengi ya kukera ikiwemo kuchagua watu wa kufanya nao kazi. Milovan alitua Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kama yeye na alipofika hapa akakabidhiwa watu wa kufanya nao kazi na akawakubali.
  Haya, Papic alimkataa kwa nini Minziro hata leo anafanya naye kazi baada ya kurejea Yanga?
  Hizo blah blah zake, madoido na mbwembwe sidhani kama ni vitu ambavyo Yanga wanavihitaji zaidi ya matokeo mazuri. Kwa sababu yuko tofauti sana na Mserbia mwenzake, Milovan.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: TOFAUTI YA PAPIC WENU NA MILOVAN WAO... Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top