• HABARI MPYA

    Friday, March 30, 2012

    WABUNGE SITA KUONGOZANA NA SIMBA ALGERIA


    WABUNGE 6 akiwemo Menyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Rage watakuwepo Setif nchini
    Algeria kushuhudia mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho kati ya Simba na ES Setif mwishoni mwa wiki ijayo.
    Akizungumza na gazeti la Habari Leo jana, Rage ambaye pia ni Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), aliwataja wabunge wengine wa Tanzania kuwa ni Khalifa Suleiman Khalifa (Gando-CUF), Murtaza Mangungu (Kilwa Kaskazini- CCM) na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini-Chadema).
    "Zitto amenieleza ataungana nasi Algeria akitokea Nigeria, pia atakuwepo Hasnain Murji na Mussa Azzan 'Zungu' (Ilala-CCM), ambaye naye atajiunga nasi akitokea Morocco.
    "Tumejipanga vya kutosha, ninaamini vijana watapata hamasa ya kutosha na mambo yatakuwa mazuri zaidi, tuna matumaini makubwa tutafanya vizuri," alisema Rage.
    Aliwaomba mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi Jumamosi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Simba na African Lyon ili kuwapa nguvu wachezaji ya kwenda kufanya vizuri Algeria.
    Alisema Simba inatarajiwa kuondoka Dar es Salaam Jumatatu na italala Cairo, Misri na siku inayofuata itaanza safari ya kwenda Algeria, ambapo wenyeji wao wamewajulisha mchezo
    utafanyika mji wa Setif.
    “Kutoka Algiers hadi Setif hapo itakuwa jukumu la wenyeji kutugharamia, maana taratibu
    za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) zinasema ikizidi Kilometa 200 itabidi usafiri unaotumika uwe wa ndege, sasa kutoka Algiers hadi Setif ni zaidi ya Kilometa 200,” alisema Rage.
    Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo wa kwanza raundi ya kwanza Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Seti Jumapili Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ambapo ili isonge mbele inahitaji ushindi wa aina yoyote, au sare ya aina yoyote ama isifungwe zaidi ya bao 1-0.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: WABUNGE SITA KUONGOZANA NA SIMBA ALGERIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top