• HABARI MPYA

    Friday, March 30, 2012

    CHAMA JOGOO AJIVUA UYANGA, AWAPA MBINU SIMBA

    Chama kulia akiwa na Juma Pondamali anayemfuatia, Marcio Maximo na James Kisaka

    'MKOBA' wa zamani wa Yanga, Athuman Juma Chama 'Jogoo' amewataka wachezaji wa Simba kutobweteka na ushindi walioupata Dar es Salaam dhidi ya Entente Setif ya Algeria.
    Simba imejiweka katika hatua nzuri ya kusonga mbele kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho baada ya kuicharaza ES Setif ya Algeria kwa mabao 2-0, mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wikiendi iliyopita.
    Chama aliyepata umaarufu kwa 'kumkaba' mshambuliaji wa Simba miaka ya 80, Zamoyoni Mogella hata kushindwa kufunga, alisema kuwa wachezaji wa Simba hawapaswi hata kidogo kuvimba vichwa na kujiona kana kwamba tayari wamemaliza kazi bali kujituma zaidi kwenye mchezo wa marudiano.
    "Nadhani kazi iliyopo mbele yao ni kubwa kuliko wanavyofikiri wao, nafikiri wanatakiwa kufahamu hilo mapema." alisema Jogoo.
    Wakati Chama akisema hayo, kocha wa Simba, Milovan Cirkovic ametabiri kuwa mchezo huo wa marudiano utakaopigwa mji wa Setif nchini Algeria April 6, mwaka huu utakuwa mgumu tofauti na ilivyokuwa Dar es Salaam.
    "Lazima tujiandae kikamilifu kabla ya mchezo wa marudiano, nafikiri wapinzani wetu watabadilika kiuchezaji tofauti na ilivyokuwa Dar es Salaam." alisisitiza Milovan.
    Chama alisema: "Viongozi wanatakiwa kuanza mikakati ya kuiandaa timu mapema, nafikiri hatua ambayo Simba wamepiga kwa sasa ni nzuri hivyo tusinge furahi kusikia au kuona tunatolewa kwenye hatua tuliyofikia kwa sasa." alisisitiza.
    Alisema maandalizi ya timu ni kitu muhimu sana na pia wachezaji wanatakiwa kuweka akili zao zote kwenye mchezo huo ili kuiwakilisha vema Tanzania kwenye michuano hiyo ikiwa Simba ni timu pekee iliyokusalia kwenye michuano ya kimataifa.
    "Waarabu ni watu ambao wanajua sana fitna za soka, tunatakiwa kujipanga imara kukabiliana nao, wakiwa nyumbani wana mbinu chafu sana za ushindi." aliongeza.
    Pia, alishauri kikosi hicho kutocheza mchezo wa kujihami zaidi kama ilivyo kwa wapinzani wao walivyocheza Dar es Salaam.
    "Kujihami kunatoa nafasi kubwa kwa adui kutengeneza mashambulizi na kushambuliaji, tucheze mpira wa kawaida tukifahamu tunatakiwa kulinda ushindi wetu na pia kushinda kama nafasi zitapatikana." alisisitiza Jogoo.

    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CHAMA JOGOO AJIVUA UYANGA, AWAPA MBINU SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top