• HABARI MPYA

    Saturday, March 31, 2012

    AGUERO NJE MAN CITY IKIIVAA SUNDERLAND LEO, MANCINI ALIA NI UPUMBAVU MTUPU, TEVEZ APEWA 90 ZOTE


    Aguero

    WAGOMBEA taji la ubingwa wa Ligi Kuu ya England, Manchester City watamkosa mshambuliaji wao Sergio Aguero katika mchezo wa leo nyumbani dhidi ya Sunderland baada ya kupata majeruhi ya kipumbavu mguuni, kocha Roberto Mancini alisema jana.
    "Ni majeruhi ya kipumbavu,"alisema Mancini katika mkutano na waandishi wa habari. "Halikuwa kosa lake, lakini hawezi kucheza na majeruhi haya; kwa siku moja, siku 10 au wiki mbili, sifahamu."
    Mancini, ambaye tayari anaye Muargentina mwenzake Aguero, Carlos Tevez hakuelezea kwa undani kuhusu majeruhi hayo.
    "Nimesikitishwa mno, natumai, (si wiki kadhaa) kwa sababu tumempoteza mshambuliaji wetu hodari kwa mambo ya kipumbavu. Hawezi kucheza dhidi ya Stoke na hawezi kucheza kesho (leo). Natumai atakuwa tayari kwa ajili ya Arsenal mwishoni mwa wiki ijayo."
    City, ambayo inazidiwa pointi tatu na Manchester United, inaweza kurejea kileleni ikiifunga Sunderland kwa sababu United hawachezi hadi Jumatatu dhidi ya Blackburn Rovers ugenini.
    Tevez amecheza mechi mbili akitokea benchi tangu arudishe uhusiano mzuri na klabu yake baada ya kutofautiana kwa kugoma kuinuka kupasha aingie kucheza mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Bayern Munich, Septemba mwaka jana na Mancini amesema mchezaji huyo anaweza kuisaidia timu katika kampeni ya ubingwa kwenye mechi nane zilizobaki.
    "Anaimarika taratibu, lakini nafikiri anaweza kuanza,"alisema Mancini. "Lakini nafikiri anaweza kucheza kwa muda zaidi, anaimarika kila wiki."
    City pia itampokea tena beki wake Vincent Kompany aliyekosa mechi nne zilizopita kwa maumivu ya nyama.
    Mbelgiji huyo ameandika kwenye akaunti yake ya Twitter kwamba: "Nimepata awamu ya pili ya mazoezi na timu. Kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa nitakuwepo kwenye mechi na Sunderland."
    Pia amewataka mashabiki wa City kuwa nyuma ya timu yao kuisaidia itwae taji la kwanza tangu mwaka 1968.
    "Ni mechi nane zilizobaki za msimu, natumai mashaiki wapo tayari kupiga kelele kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku zote na tutahakikisha tunafanya mambo mazuri," alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AGUERO NJE MAN CITY IKIIVAA SUNDERLAND LEO, MANCINI ALIA NI UPUMBAVU MTUPU, TEVEZ APEWA 90 ZOTE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top