• HABARI MPYA

    Saturday, March 31, 2012

    SIMBA, YANGA KAZINI LIGI KUU BARA LEO




    TIMU za Simba na Yanga ambazo zinachuana vikali kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, leo zitakuwa kwenye viwanja viwili tofauti kusaka pointi tatu muhimu ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu.
    Katika mechi hizo za raundi ya 22 mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga watakuwa wanakaribishwa jijini Tanga na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, kwenye mchezo ambao umekuwa gumzo kwa wiki nzima.
    Malumbano hayo yalitokana na uamuzi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Tibaigana kusitisha kwa muda adhabu walizopewa baadhi ya wachezaji nyota wa Yanga, jambo ambalo lilichukuliwa kama hujuma na klabu ya Coastal Union.
    Kwani uamuzi huu ulionekana utaifaidisha Yanga katika mchezo huo wa leo.
    Simba ambayo inaongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 47, leo itakuwa inajitupa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuumana na African Lyon .
    Simba nayo itakuwa ikisaka pointi tatu ili kujiimarisha kileleni mwa ligi hiyo pamoja na kuweka hai matumaini yao ya kuwapoka ubingwa watani zao Yanga, ambao wako nafasi ya tatu wakiwa na pointi 43.
    Wakati huo huo, uamuzi wa Kamati ya Nidhamu ya TFF kuhusiana na adhabu walizopewa wachezaji wa Yanga kutokana na kitendo cha kumpiga mwamuzi Israel Nkongo katika mchezo wao dhidi ya Azam sasa utatolewa Jumanne ijayo.
    Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa awali uamuzi huo ulitarajiwa kutolewa juzi, lakini sasa kikao cha Kamati ya Tibaigana kitafanyika Jumanne wiki ijayo.
    Wambura alisema kikao hicho kimepangwa kufanyika siku hiyo ili kutoa nafasi kwa Yanga pamoja na wachezaji hao kufika kutoa maelezo yao mbele ya Kamati.
    Kutokana na hali hiyo, Wambura alisema wachezaji wote wa Yanga waliokuwa wamefungiwa na kisha Tibaigana kusitisha adhabu zao Jumamosi iliyopita wataruhusiwa kucheza mechi ya leo dhidi ya Coastal Union.
    Wachezaji hao ni Stephano Mwasika aliyefungiwa mwaka mmoja, Jerry Tegete miezi sita, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mechi sita na Omega Seme na Nurdin Bakari, waliofungiwa mechi
    tatu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA, YANGA KAZINI LIGI KUU BARA LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top