• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 27, 2012

  PATASHIKA ULAYA ROBO FAINALI YAANZA

  HUKU Ligi ya Mabingwa Ulaya ikifikia hatua tamu ya robo fainali, ni wazi kuwa klabu zimekuwa na wasiwasi juu ya wapinzani wao, lakini hali ni tofauti kwa kocha wa Benfica, Jorge Jesus ambaye amesema mechi ya leo Jumanne dhidi ya Chelsea ni kicheko kwake.
  Benfica inakutana na Chelsea ikiwa na historia ya kutoka suluhu na Olhanense na hivyo kuendelea kuwa katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Ureno, nyuma ya Porto.
  �Siwezi kuficha hisia zangu, ninafurahi kukutana na Chelsea," alisema kocha huyo.
  Lakini huenda wasiwe na mteremko kama wanavyofikiria kwa sababu Chelsea sasa inaendelea vizuri chini ya kocha mpya Roberto Di Matteo. Licha ya kwamba wiki iliyopita walifungwa na Manchester City mabao 2-1, wikiendi iliyopita walitoka suluhu na Tottenham.
  Na baada ya mechi hiyo, Di Matteo alisema kuwa anataka kushinda katika mechi zote zilizobaki. Lakini kama watafanikiwa kuimaliza Benfica watakutana na Barcelona au AC Milan katika nusu fainali.
  Wakati makocha hao wakitambiana, kesho Jumatano kutakuwa na mchezo wa 'kukata na shoka' kati ya AC Milan na Barcelona katika Uwanja wa San Siro.
  Na wakati AC Milan na Barcelona wakisubiriana katika mechi hiyo kuna mechi nyingine ya Goliati na Daudi ambayo ni kati APOEL Nicosia na Real Madrid.
  Kama APOEL itashinda leo Jumanne itakuwa ni jambo la kushtua na kama AC Milan itashinda dhidi ya Barca itakumbusha fainali ya 1994 wakati timu ya Italia iliposhinda mabao 4-0.
  Lakini mabingwa mara saba wa Ulaya, AC Milan wanakabiliwa na majeruhi na wataingiza kikosi uwanjani bila ya Thiago Silva, beki wa kati aliyetarajiwa 'kula sahani moja' na Lionel Messi.
  Messi yupo katika kiwango cha juu, amefunga mabao 18 katika mechi tisa zilizopita na aliwasha moto wakati Barcelona iliposhinda mabao 7-1 dhidi ya Bayer Leverkusen kwenye hatua ya mtoano.
  Nayo Bayern Munich iliitungua FC Basel mabao saba katika hatua ya 16 bora na kuondoa matumaini ya timu hiyo ya Uswisi kuingi robo fainali kwa mara ya kwanza.
  Timu hiyo itakutana na Marseille, ambayo imeingia robo fainali kwa mara ya kwanza tangu 1993. Mechi zote zitaanza saa 4:45 na zitaonyeshwa live na Super Sport TV.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: PATASHIKA ULAYA ROBO FAINALI YAANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top