• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 29, 2012

  NSA AIONDOA ENEO BAYA VILLA, MTIBWA YACHAKAZWA JESHINI


  Nsa aliyebinuka tik tak enzi zake akiwa Yanga

  MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Nsa Job ameendelea kufunga mabao Ligi Kuu ya Bara, baada ya jana pia kuifungia timu yake, Villa Squad katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Moro United, Uwanja wa Chamazi.
  Kwa matokeo hayo, Villa imepanda kutoka nafasi ya mwisho mkiani hadi nafasi ya 12 na kuishusha Moro United kwa nafasi moja.
  Villa imefikisha pointi 19 na Moro 18, nafasi ya 14 sasa inashikiliwa na Polisi Dodoma yenye pointi 17.
  Timu hizo tatu zinapigania 'uhai' wa kubaki kwenye ligi hiyo kwani zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
  Bao la Moro United lilifungwa na Rajab Zahir katika dakika ya 44.
  Mabao ya Villa yalifungwa na Nsa katika dakika ya 23 na Omari Issa dakika ya 90.
  Katika mchezo mwingine, Mtibwa Sugar jana ilichezea kichapo ugenini kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Ruvu Shooting.
  Matokeo hayo yameifanya Mtibwa iendelee kubaki nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 34, huku Ruvu Shooting ikibaki nafasi ya nane baada ya kufikisha pointi
  27.
  Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute Ruvu ilipata mabao yake kupitia kwa Hassan
  Dilunga aliyefunga mawili dakika ya 34 na 47 na Mohamed Kijuso alifunga katika dakika ya 43.
  Kwa upande wa Mtibwa Sugar ilipata bao lake la kufutia machozi kupitia kwa Thomas Mourice
  dakika ya 90.
  Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena mwishoni mwa wiki hii ambapo vigogo wa soka nchini
  Simba na Yanga watakuwa kwenye viwanja viwili tofauti kuendeleza mbio za kuwania ubingwa.
  Yanga inayotetea ubingwa itakuwa ngeni wa Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani
  Tanga na Simba itakuwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam ikiikaribisha African Lyon.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: NSA AIONDOA ENEO BAYA VILLA, MTIBWA YACHAKAZWA JESHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top