• HABARI MPYA

  Jumanne, Machi 27, 2012

  JULIO AWACHIMBIA MKWARA YANGA

  Julio
  KOCHA mkuu wa Coastal Union ya Tanga, Jamhuri Kihwelo 'Julio' amesema kikosi chake kitavuruga mipango ya Yanga inayotaka kuigeuza timu yake ngazi ya kutwaa ubingwa.
  Yanga na Coastal Union 'Wagosi wa Kaya' zitakwaana katika mchezo wa ligi kuu unaotarajiwa kuwa mgumu utakaopigwa Machi 31 kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
  Kauli ya Julio imekuja kufuatia uamuzi wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF)kutangaza kusimamisha kwa siku 14 adhabu ya kufungiwa iliyowakumba wachezaji watano wa Yanga baada ya kamati inayosimamia ligi kuu kuwatia hatiani kwa kosa la kumpiga mwamuzi Israel Nkongo  wakati wa mechi dhidi ya Azam iliyochezwa uwanja wa Taifa Machi 10.
  Nyota waliofungiwa na hatimaye kufunguliwa kwa muda na kamati hiyo iliyo chini ya uenyekiti wa Alfred Tibaigana ni pamoja na Stephano Mwasika aliyefungiwa mwaka mmoja, Jerryson Tegete (miezi sita) Nadir Haroub(Mechi sita) pamoja na Nurdin Bakar na Omega Seme waliosimamishwa mechi tatu. 
  Akizungumza kwa simu kutoka Tanga, Julio alisema kurejea kwa nyota hao kumeongeza morali ya wachezaji wake ambao wameapa kufia uwanjani ili mradi ushindi upatikane.
  "Nikuambie kitu kimoja bwana, wachezaji wa Tanzania hawatofautiani, walioko Yanga na hawatofautiani walioko Coastal Union ni wale wale isipokuwa tatizo ni hii tabia yetu yakutaka timu fulani tu ndo ziwe bingwa.
  "Tena nashukuru kama watakuja na hao  wanaowaona wana umuhimu ili tunakapowafunga isionekana kwa sababu hawakuwa na wachezaji fulani, lakini nataka kukuambia kwamba Yanga hawajawahi kunifunga na huo wote ni mchecheto,"alisema Julio.
  Alizungumzia uamuzi wa kamati hiyo ya nidhamu na usuluhishi ya kusimamisha adhabu kwa wachezaji hao watano wa Yanga kwa kudai kuwa:
  "Hasikuambie mtu bwana, kitendo kilichofanywa na Tibaigana cha kuwafungulia wachezaji waliompiga mwamuzi kina lengo la kuisaidia Yanga.
  "Naapa kwamba mipango yao haitafanikiwa, jambo la msingi mwamuzi  atakayekuja kuchezesha pambano letu achezeshe kwa haki achezeshe kwa haki vinginevyo tutampiga ili tuone kama na sisi tutafungiwa," alisema Julio na kusisitiza kwa amekerwa sana na uamuzi wa kamati hiyo.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: JULIO AWACHIMBIA MKWARA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top