• HABARI MPYA

  Alhamisi, Machi 29, 2012

  REBECCA MALOPE KUTUA APRILI 6


  Rebecca Malope

  MALKIA wa muziki wa Injili nchini Afrika Kusini, Rebecca Malope, anatarajia kuwasili nchini Aprili 6 mwaka huu, ili kutumbuiza katika tamasha la nyimbo za Injili la Pasaka litakalofanyika Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
  Akizungumza Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha hilo chini ya Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, Alex Msama, alisema Rebecca anatarajia kuwasili na kundi la wanamuziki wake 13.
  "Rebecca ameahidi atapiga 'live' akishambulia jukwaa kwa takriban saa 2 na ushei na atapiga nyimbo zake mpya tano na nyingine za zamani," alisema Msama.
  Akizungumza kwa njia ya simu wiki hii kutoka Afrika Kusini, Rebecca aliahidi kuwaletea Watanzania zawadi ya Pasaka, na akabainisha ataambatana pia na waimbaji wengine kutoka Afrika Kusini.
  Rebecca alisema amewaandalia zawadi nzuri mashabiki wa muziki wa Injili wa Tanzania, na akatoa mwito wajitokeze kwa wingi siku ya tukio ili kumshuhudia.
  "Naahidi kuwaletea Watanzania zawadi ya Pasaka... nimewaandalia vitu vipya ambavyo naamini watavifurahia," alisema Rebecca.
  Rebecca aliyezaliwa katika shamba la tumbaku Afrika Kusini, alisema katika tamasha hilo la Pasaka mwaka huu ataimba nyimbo mbalimbali zilizomo kwenye albamu zake, zikiwemo tano mpya.
  Rebecca amewahi kutamba na albamu za Saturday Nite (aliyoitoa Januari 1, 2009), Hlala Nami (Novemba 11, 2003), Siyabonga (Desemba 21, 2000), Free at Last (Novemba 18, 1997), African Classics (Mei 5, 2009) na Greatest Hits (Januari 10, 2006).
  Malope atakuwa mmoja kati waimbaji siku hiyo wakiwemo Rose Muhando, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti Faraja Ntaboba, Ephraim Sekeleti, Maryanne Tutuma, kundi la Glorious Celebration na kwaya ya Kinondoni Revival.
  Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu ambako mgeni rasmi atakuwa Naibu Spika, Job Ndugai.
  Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake wajane.
  Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti maalumu sh. 10,000.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: REBECCA MALOPE KUTUA APRILI 6 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top