• HABARI MPYA

  Jumatano, Machi 28, 2012

  YANGA WASEMA NA WANANCHI

  MSHAMBULIAJI wa Yanga ya Dar es Salaam Jerry Tegete, amesema mashabiki wa soka nchini waache kuwashutumu na kuwaona kama watu wasiostahili kwenye jamii.
  Akizungumza kwa simu na gazeti la Habari Leo jana, Tegete alisema tangu watangazwe kufungiwa na hata ulipotolewa uamuzi wa kusitishwa kwa muda adhabu yao, mashabiki wamekuwa wakiwahukumu na kuwaona si watu wa kawaida.
  “Kila siku watu wanatoa maoni yao, mara Tegete hivi, mara Mwasika vile, jamani sisi pia ni wanadamu, inafikia wakati yanakera.
  “Sasa juzi imetangazwa kwamba adhabu yetu inasitishwa kwa muda, watu hata hawajui kanuni zinasemaje wameanza kulalamika kwa nini iwe hivi, kwa nini wanaachiwa, si msome kanuni ndipo mtoe maoni yenu?” Alihoji Tegete.
  Hivi karibuni Kamati ya Ligi ya TFF, iliwafungia wachezaji watano wa Yanga kutokana na kudaiwa kuhusika na vurugu kwa kumpiga mwamuzi Israel Nkongo wakati wa mchezo wa Yanga na Azam wiki mbili zilizopita, ambao Yanga ilifungwa mabao 3-1.
  Wachezaji hao ni Stephano Mwasika aliyefungiwa mwaka mmoja, Jerry Tegete miezi sita, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mechi sita, Omega Seme na Nurdin Bakari, waliofungiwa mechi
  tatu.
  Lakini mwishoni mwa wiki iliyopita, Mwenyekiti wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya TFF, Alfred Tibaigana ambaye amepata kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, alisitisha adhabu hiyo kwa kutumia mamlaka aliyopewa na kanuni ya 129 ya Kanuni za adhabu za Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
  Tibaigana aliamuru kusitishwa kwa adhabu zilizotolewa na Kamati ya Ligi ya TFF kwa wachezaji wa Yanga, ambapo chini ya Kanuni hiyo, Mwenyekiti anayo mamlaka ya kusitisha utekelezaji wa adhabu yoyote ile pale anapoona kwamba ukiukwaji unaolalamikiwa hautaweza kupatiwa ufumbuzi wa haraka bila kuathiri haki za wale wanaokata rufani,” alisema Wambura.
  Alisema usitishwaji wa adhabu hizo, ambao utadumu kwa muda wa siku 14, kuanzia tarehe ya kusitishwa huko, una nia ya kutoa fursa kwa sekretarieti ya TFF kuwasilisha rufani ya Yanga pamoja na maelezo yanayohusiana na rufani hiyo, mbele ya Kamati yake ili isikilizwe na hatimaye kuitolea maamuzi.
  Pia Kamati hiyo iliiagiza TFF ifanye juhudi za kuharakisha usikilizwaji wa rufani hiyo ili kuwawezesha wachezaji waliohusika kujua hatma yao kimichezo.
  Akizungumzia hilo Tegete alisema anashukuru kwamba Tibaigana ameliona hilo na kwamba wanasubiri muda huo ili rufani zao zisikilizwe na ndipo mashabiki wanaweza kutoa maoni.
  Kwa upande wake Mwasika alipoombwa kuzungumzia suala hilo jana, alisema kwa sasa hayupo tayari kufanya hivyo mpaka Kamati ya Tibaigana itakapomaliza kazi yake kwani kufanya hivyo kutaibua maneno mengi yasiyo na msingi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA WASEMA NA WANANCHI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top