• HABARI MPYA

    Tuesday, March 20, 2012

    MTIBWA, SIMBA WAINGIZA MILIONI 31 JAMHURI


    MCHEZO namba 146  wa  Ligi Kuu ya Vodacom baina ya  Mtibwa Sugar na Simba uliochezwa  Machi 18 mwaka huu katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro umeingiza sh. 31,230,000.
    Ofisa habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura alisema jana kwamba fedha hizo zimepatikana kupitia watazamaji 10,410 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo kwa kiingilio cha sh. 3,000.
     “Baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 4,763,898.31 kila timu ilipata sh. 6,508,230.51, uwanja sh. 2,169,410.17,Chama cha soka Mkoa wa Morogoro (MRFA) sh. 867,764.07, TFF  sh. 2,169,410.17, Mfuko wa Maendeleo wa soka (FDF) sh. 1,084,705.08, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 216,941.02 na asilimia 10 ya gharama za mechi sh. 2,169,410.17”, Alisema Wambura.
    Katika hatua nyingine timu za Villa Squad na JKT Ruvu leo zitahitimisha raundi ya 21 ya ligi hiyo kupitia mchezo wao utakaopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, jijini Dar es Salaam.
    Aidha Machi 24 mwaka huu kutakuwa na mechi ya ligi hiyo kati ya Moro United na African Lyon itakayopigwa pia kwenye dimba la Chamazi, kabla ya Machi 28 mwaka huu  Ruvu Shooting Stars itakwaana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Moro United itakuwa mwenyeji wa Villa Squad itakayofanyika Uwanja wa Chamazi.
    Wakati huo huo: Mkutano Mkuu wa kawaida wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) uliokuwa ufanyike Machi 24 na 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam umesogezwa mbele hadi Aprili 21 na 22 mwaka huu.
    Ofisa Habari wa TFF Boniface Wambura alisema jana kwamba Kamati ya Utendaji ya Shirikisho hilo iliyokutana Machi 10 mwaka huu jijini Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Leodegar Tenga uliamua kusogeza mbele Mkutano Mkuu kutokana na mtiririko wa matukio ndani ya TFF katika kipindi hicho.
    Alisema katika mkutano huo mkuu kutakuwa na ajenda 25 mbalimbali katika Mkutano Mkuu huo wa kawaida wa TFF zikiwemo kufungua kikao, kuthibitishwa kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu, kuthibitisha muhtasari wa Mkutano Mkuu uliopita na  yatokanayo na muhtasari wa kikao kilichopita.
    Pia kutakuwa na  hotuba ya Rais, kupokea taarifa za utekelezaji za wanachama na kupokea taarifa ya utekelezaji ya Kamati ya Utendaji,  kupitisha taarifa ya ukaguzi wa hesabu za mwaka uliopita, kupitisha taarifa ya wakaguzi wa hesabu na hatua zilizochukuliwa na  kupitisha bajeti ya mwaka 2012.
    “Ajenda nyingine ni  kupitisha mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya TFF, kujadili mapendekezo yaliyowasilishwa na Wanachama au Kamati ya Utendaji, mengineo na kufunga kikao,”Alisema Wambura.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MTIBWA, SIMBA WAINGIZA MILIONI 31 JAMHURI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top