MWIMBAJI wa muziki wa Injili kutoka Kenya, Maryanne Naipasoi
Tutuma amethibitisha kushiriki tamasha la Pasaka litakalofanyika Sikukuu ya
Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex
Msama ambaye ni Mkurugenzi wa Msama Promotions, waandaaji wa tamasha hilo,
alisema Maryanne amekubali kushiriki.
Msama alisema Dar es Salaam jana kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo
za kumsifu Mungu atatua nchini akiwa na albamu yake ya Ilmaasae Asai aliyoiimba
kwa lugha ya Maasai.
Baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa, mashambulizi mengine
yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka huu.
Aliongeza kwamba Maryanne atakuja nchini na waimbaji wake na
ataimba 'live' siku hiyo ambayo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu lina malengo ya kuchangisha
fedha kwa ajili ya watoto yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane
wasiojiweza.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria
tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti
maalumu sh. 10,000.
Mbali na Maryanne, wasanii wengine wa nyimbo za Injili
watakaopamba tamasha hilo ni Rebecca Malope, Rose Muhando, Christina Shusho,
Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa, Anastazia Mukabwa, Atosha
Kissava, Ephraim Sekeleti na kundi la Glorious Celebration.
Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival inayotamba na albamu
yao mpya ya Mtu wa Nne, inatarajia kutumbuiza katika tamasha la Pasaka na
Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka DRC.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu litashirikisha waimbaji wa
nyimbo za Injili kutoka nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Congo, Afrika Kusini na Zambia.


.png)
0 comments:
Post a Comment