• HABARI MPYA

  Friday, March 29, 2024

  YANGA KUIVAA MAMELODI BILA DIARRA, YAO, AUCHO WALA PACOME


  KOCHA Muargentina wa Yanga SC, Miguel Ángel Gamondi amethibitisha katika mchezo wa kesho dhidi ya Mamelodi Sundowns atawakosa nyota wake wanne, mabeki Kibwana Shomari, Kouassi Attohoula Yao (Ivory Coast)na viungo Peadoh Pacome Zouazoua (Ivory Coast) na Khalid Aucho (Uganda) ambao wote ni majeruhi.
  Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Miguel Ángel Gamondi pia hana uhakika wa kuwatumia kipa Djigui Diarra (Mali) na kiungo Stephane Aziz Ki (Burkina Faso) katika mchezo huo kwa sababu hadi mchana wa leo walikuwa hawajarejea nchini kutoka kwenye majukumu ya timu zao za taifa.
  “Natarajia kuwakosa baadhi ya wachezaji wangu nyota. Siwezi kuhatarisha afya za wachezaji ambao bado hawana utimamu wa kimwili. Lakini kuna uwezekano mkubwa wa kuwakosa wachezaji watatu hadi wanne,”amesema Gamondi.
  Pamoja na hayo, Muargentina huyo pamoja na kuwakosa nyota hao, lakini ana imani na wachezaji wengine walio fiti baada ya manadalizi mazuri kambini Avic Town, Kigamboni kwa wiki takriban mbili watafanya vizuri.
  Yanga watakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kesho kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana  Ijumaa ya Aprili 5 Uwanja wa Loftus Jijini Pretoria.
  Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 na Mamelodi Sundowns wakaitoa Yanga kwa jumla ya mabao 6-5, wakishinda 3-2 Pretoria na kutoa sare ya 3-3 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
  Mshindi wa jumla baina ya Yanga na Mamelodi Sundwons atakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA KUIVAA MAMELODI BILA DIARRA, YAO, AUCHO WALA PACOME Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top