• HABARI MPYA

  Saturday, March 23, 2024

  MENEJA AIELEZA MAHAKAMA MWANAMUZIKI LAMECK DITTO AMEKOSESHWA SH. BILIONI 1.8  Lameck Ditto (mwenye kofia) akijadiliana jambo na wakili wake, Elizabeth John na meneja wake Rodney Rugambo (mwenye fulana nyeupe) nje ya court ya Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam.

  KESI ya Madai baina ya mwanamuziki Lameck Ditto na kampuni ya MultiChoice Tanzania Limited iliendela kusikilizwa jana katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam.
  Meneja wa mwanamuziki huyo, Rodney Rugambo aliieleza Mahakama Kuu hiyo namna ambavyo Lameck Ditto aliathirika baada ya wimbo wake wa Nchi Yangu kutumiwa na MultiChoice Tanzania Limited kwenye matangazo yao ya biashara kipindi cha Kampeni ya Afcon 2019.
  Akitoa ushahidi wake, mbele ya jaji mfawidhi, Salma Maghimbi jana, Rodney ambaye ni shahidi wa nne kati ya watano  katika kesi hiyo ya madai, alisema amekuwa meneja wa Ditto tangu mwaka 2016.
  Alisema, mwaka 2017, Ditto aliandika wimbo huo, wakilenga kuutumia kama nembo (brand) kwenye kampeni ya Kibanda umiza.
  "Wimbo ulipotengenezwa, tulikuwa na mpango wa kuitumia kwenye kampeni ya Kibanda umiza," alisema.
  Katika ushahidi wake, alidai kwenye kampeni hiyo, katika kipindi cha miaka mitano, Ditto angelipwa Sh 1.8bilioni.
  Alisema, kabla ya kuanza kwa kampeni hiyo, waratibu wa Tamasha la urithi, waliuomba kuutumia kwenye tamasha hilo.
  "Kwenye tamasha la urithi wimbo huo haukutumika kwa ajili ya kibiashara, tukiwa tunaendelea na mchakato wa kuutumia kwenye kampeni ya Kibanda umiza,  tulishangaa kuona DSTV (Kampuni ya
  MultiChoice Tanzania Limited) wameutumia kwenye matangazo yao ya kibiashara," alisema meneja huyo.
  Alisema, jambo lile lilimuathiri Ditto ambaye hakuweza kuendelea kwenye kampeni ya Kibanda Umiza.
  "Wimbo wa Nchi yangu haukutumiwa tena kwenye kampeni ile na yeye (Ditto) kushindwa kuendelea na mkataba ule, kwani tayari wimbo ulishatumika kibiashara na kampuni nyingine hivyo thamani yake kushuka," alisema Rodney.
  Baada ya kutoa ushahidi wake, mawakili wa Multi Choice Thomas Mathias na Lyimo walimuuliza maswali kadhaa shahidi huyo, ikiwamo endapo anafahamu kuhusu mashindano ya Afcon na shahidi huyo kueleza hajui chochote kuhusu mpira wa miguu.
  Ditto ambaye jina lake halisi ni Dotto Bernard Bwakeya alifungua kesi ya madai Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam mwaka 2020 akiomba iamuru kampuni Multi Choice Tanzania imlipe fidia ya Sh 6bilioni kwa kutumia wimbo  wa Nchi Yangu aliodai ni wake kwenye matangazo yao ya biashara bila ridhaa yake.
  Pia ameiomba Mahakama iamuru alipwe Milioni 200 kutokana na madhara ya jumla, pia alipwe riba ya asilimia 25 tangu siku alipofungua shauri hilo akidai kampuni hiyo imemnyima fursa ya kunufaika na kazi yake.
  Kesi hiyo itaendelea tena Jumatatu, Machi 25 kwa shshidi watano kutoa ushahidi wake Mahakamani hapo, upande wa mshtaka ukiongozwa na mawakili Ally Hamza na Elezabeth John.


  Lameck Ditto (mwenye kofia) baada ya kuwasili Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam na Meneja wake.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MENEJA AIELEZA MAHAKAMA MWANAMUZIKI LAMECK DITTO AMEKOSESHWA SH. BILIONI 1.8 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top