• HABARI MPYA

  Wednesday, March 20, 2024

  HUSSEIN ITABA KUPIGANA PAMBANO LA EDDIE HEARN JUMAMOSI UINGEREZA


  Bondia Hussein Itaba atapanda tena ulingoni Jumamosi ya Machi 23 kuzipiga na Muingereza mwingine, Liam Cameron ukumbi wa Sheffield Arena, Sheffield, Yorkshire pambano linalondaliwa na promota Eddie Hearn

  KAMPUNI ya MHD Promotions ya Uingereza imeamua kumchukua bondia Hussein Itaba wa Tanzania baada ya kuvutiwa na uwezo wake akipigana na mwenyeji, Thomas O'Toole Jumamosi ya Machi 16 ukumbi wa Salthill Leisureland Complex, Galway nchini Ireland.
  Itaba alipoteza kwa pointi pambano hilo la uzito wa Light Heavy, ingawa macho ya wengi yaliona Mtanzania huyo ndiye kashinda - na baada ya mchezo huo Promota Mark Dunlop amemuambia Itaba abaki kwa ajili ya pambano lingine.
  Watanzania wengine wawili walipanda ulingoni siku hiyo, Tampela Maharusi akipoteza pia kwa pointi mbele ya Colm Murphy uzito wa Feather na Godfrey Paulo Kamata akapigwa kwa Technical Knockout (TKO) Raundi ya sita na Luke Keeler uzito wa Light Heavy.
  Wakati Maharusi na Kamata wanarejea nyumbani, Itaba amebaki Ireland kwa ajili ya pambano lingine chini ya MHD Promotions dhidi ya Liam Cameron Jumamosi ya Machi 23 ukumbi wa Sheffield Arena, Sheffield, Yorkshire, Uingereza.


  Itaba atapigana katika mapambano yanayoandaliwa na Promota mkubwa Uingereza, Edward ‘Eddie’ John Hearn wa kampuni ya Matchroom Boxing, ambaye amekuwa akiwapromoti akina Anthony Joshua, Canelo Álvarez, Gennady Golovkin, Oleksandr Usyk, Vasyl Lomachenko, Katie Taylor na wengine wengi.
  Siku hiyo, pambano Kuu ni baina ya Muingereza, Dalton Smith na Mmarekani Jose Zepeda watakaowania taji la WBC Silver uzito wa Super Light ambalo lipo wazi.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HUSSEIN ITABA KUPIGANA PAMBANO LA EDDIE HEARN JUMAMOSI UINGEREZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top