• HABARI MPYA

    Wednesday, March 20, 2024

    SERIKALI YASISITIZA UZALENDO SIMBA NA YANGA DHIDI YA AHLY NA MAMELODI ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA


    WAZIRI wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro amewaomba Watanzania  waziunge mkono Simba na Yanga kwenye michezo ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri na Mamelodi Sundowns ya Afrika ili zishinde na kuiletea heshima kwa nchi. 
    Aidha, amewaonya baadhi ya Watanzania ambao wamekuwa na tabia ya kuzipokea na kuzishangilia timu ngeni zinapokuja kucheza na timu za Tanzania waache tabia hiyo kwa kuwa inarudisha nyuma juhudi kubwa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan ambaye katika uongozi wa miaka mitatu amefanya mambo makubwa kuendeleza michezo nchini.
    Dk. Ndumbaro ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa mtandao mpya wa Simba SC uliopewa jina la "Simba Executive Network" ambao una lengo kukusanya fedha kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya Klabu hiyo.
    "Natamani kuziona timu zote  nusu fainali, inaleta heshima kwa nchi, inaleta heshima kwa mpira wetu na vilabu vyetu,” amesisitiza Dk. Ndumbaro.
    Amesema Serikali haifurahishwi na tabia ya baadhi ya Watanzania ambao huwafanya wageni wajisikie nyumbani wanapokuja kucheza hapa nchini huku wakiibeza timu ya Tanzania jambo ambalo halina faida kwa maendeleo ya soka.
    "Timu ambayo itajigeuza kuwa Kamati ya itifaki kwenda kupokea wageni Uwanja wa ndege tutashughulika nayo, wageni watapokewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) , ndivyo taratibu zinavyoelekeza na sio timu. Kuanzia mechi hizi kiongozi yeyote,  Mwanachama au timu itakayofanya hivyo hatutaivumilia,” amesisitiza Dk. Ndumbaro. 
    Simba SC watakuwa wenyeji wa Al Ahly katika mchezo wa kwanza wa Robó Fainali Ijumaa ya Machi 29 kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana Ijumaa itakayofuata Aprili 5 Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo, Misri.
    Ikumbukwe mwishoni mwa mwaka jana timu hizo zilikutana katika Robó Fainali ya michuano mipya, African Football League na kutoa sare ya jumla ya 3-3, wakifungana 2-2 Oktoba 20 Dar es Salaam na 1-1 Oktoba 24 Cairo, hivyo Al Ahly kwenda Nusu Fainali kwa faida ya mabao ya ugenini.
    Kwa upande wao Yanga watakuwa wenyeji wa Mamelodi Sundowns Jumamosi ya Machi 30 kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam, kabla ya timu hizo kurudiana  Ijumaa ya Aprili 5 Uwanja wa Loftus Jijini Pretoria.
    Mara ya mwisho timu hizo zilikutana katika Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2001 na Mamelodi Sundowns wakaitoa Yanga kwa jumla ya mabao 6-5, wakishinda 3-2 Pretoria na kutoa sare ya 3-3 Uwanja wa CCM Kirumba Jijini Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI YASISITIZA UZALENDO SIMBA NA YANGA DHIDI YA AHLY NA MAMELODI ROBO FAINALI LIGI YA MABINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top