• HABARI MPYA

  Thursday, March 28, 2024

  BENCHIKA: TUNA KAZI NGUMU MBELE YA AHLY KESHO


  KOCHA Mkuu wa Simba SC, Mualgeria Abdelhak Benchika amesema wana kazi ngumu kesho mbele ya Al Ahly ya Misri katika mchezo wa kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
  Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam, Becnhika amesema kwamba Al Ahly ni timu nzuri na yenye uzoefu mkubwa wa michuano hiyo wao wakiwa wanashikilia taji hilo. 
  "Tuna kazi kubwa ya kwenda kufanya ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kwenye mchezo wa nyumbani na wachezaji wote wanalifahamu hilo," amesema Abdelhak Benchika.
  Kwa upande wake beki wa timu hiyo, Shomari kapombe akizungumza kwa niaba ya wachezaji amewaomba mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu ipate matokeo mazuri.
  "Tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kuja kutupa nguvu muda wote wa mchezo, kwani kutokana na maandalizi tuliyoyafanya, naamini tunakwenda kupambana na kufanya vizuri kwa kupata ushindi," amesema Shomari Kapombe.
  Simba SC watakuwa wenyeji wa mabingwa hao watetezi katika mchezo huo wa kwanza wa Robó Fainali kesho kuanzia Saa 3:00 usiku Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.
  Timu hizo zitarudiana Aprili 5 Uwanja wa Cairo International Jijini Cairo, Misri na mshindi wa jumla atakutana na mshindi wa jumla katí ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Petro de Luanda ya Angola katika Nusu Fainali.
  Ikumbukwe timu hizo zilikutana katika Robó Fainali ya michuano mipya, African Football League na kutoa sare ya jumla ya 3-3, wakifungana 2-2 Oktoba 20 Dar es Salaam na 1-1 Oktoba 24 Cairo, hivyo Al Ahly kwenda Nusu Fainali kwa faida ya mabao ya ugenini.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BENCHIKA: TUNA KAZI NGUMU MBELE YA AHLY KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top