• HABARI MPYA

  Sunday, February 05, 2023

  SENEGAL BINGWA CHAN 2023, ALGERIA YAFA KWA MATUTA ALGIERS


  TIMU ya Senegal imefanikiwa kutwaa ubingwa wa Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) 2023 baada ya ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya wenyeji, Algeria kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 120 usiku wa jana Uwanja wa Nelson Mandela, Baraki mjini Algiers.
  Baada ya dakika 120 ngumu kwa pande zote mbili, mambo yakawa meusi kwa kocha Madjid Bougherra wa Mashujaa wa Jangwani kwenye mikwaju ya penalti mbele ya Simba wa Teranga wakiongozwa na kocha Pape Thiaw.
  Waliofunga penalti za Senegal ni Elhadji Mooutarou Balde, Moussa Ndiaye, Moussa Kante, Lamine Camara na Ousmane Diouf wakati za Algeria zilifungwa na Akram Djahnit, Zakaria Draoui, Soufiane Bayazid na Youcef Laouafi.
  Kipa wa Algeria, Alexis Guendouz ndiye aliyekuwa wa kwzna kuokoa penalti jana baada ya kupangua mkwaju wa Cheikhou Omar Ndiaye, lakini bahati mbaya mwenzake, tuta la mwenzake Aimen Mahious ambaye ndiye mfungaji bora kwa mabao yake matano liliokolewa na kipa Pape Mamadou Sy na Ahmed Kendouci akakosa.
  Pamoja na hayo, Algeria imeweka rekodi mpya kwenye michuano hiyo baada ya kucheza mechi zote sita za CHAN ya mwaka huu bila kuruhusu bao katika muda wa kawaida huku mechi ya Fainali ikiwa pekee iliyofika kwenye muda wa nyongeza mwaka huu.
  Ikumbukwe Ijumaa Madagascar ilifanikiwa kushinda nafasi ya tatu baada ya ushindi wa 1-0 dhidi ya Niger, bao pekee la Jean Yves Razafindrakoto dakika ya 90 Uwanja wa Miloud Hadefi mjini Oran.
  Mabingwa wa awali wa CHAN ni 2009; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), 2011; Tunisia, 2014; Libya, 2016; DRC, 2018 na 2020 zote Morocco.

  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SENEGAL BINGWA CHAN 2023, ALGERIA YAFA KWA MATUTA ALGIERS Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top