• HABARI MPYA

    Thursday, June 07, 2018

    AFRICAN LYON WATAKA KUJUA MDHAMINI WA LIGI KUU MSIMU UJAO, WASEMA HAWATAKI KUVULIWA JEZI UWANJANI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KLABU ya African Lyon ya Dar es Salaam imelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumtaja mdhamini wa msimu ujao wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kufuatia kampuni ya Vodacom Tanzania kumaliza mkataba wake.
    Hayo yamesemwa na mmiliki wa Lyon, Rahim Kangezi ‘Zamunda’ leo katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online kutoka New York, Marekani.
    Zamunda ambaye yupo Marekani kununua vifaa vya michezo kwa ajili ya timu yake amesema kwamba ikiwa sasa ni miezi miwili kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu kuanza, ni wakati mwafaka kwa TFF kumtaja mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu.
    Rahim Kangenzi (kushoto), akiwa na kocha wa zamani wa Chelsea, Roberto Di Matteo (kulia)

    “Lazima tujue mapema mdhamini ili sisi kama klabu tusiende kuingia mikataba na wadhamini wanaofanya biashara sawa na wadhamini wa Ligi Kuu,”amesema Zamunda na kuongeza; “Hata kama Vodacom wataendelea, lazima waweke wazi ili tujue mapema nasi tuendelee na maandalizi yetu bila kugusa maslahi yao.
    “Kwa mfano sisi hapa hatuwezi kwenda udhamini kampuni au taasisi yoyote, hata iwe ya kifedha, huduma za simu, vinywaji au usafirishaji, kwa sababu hatujui mdhamini mkuu wa Ligi Kuu msimu ujao atakuwa nani. Unaweza kwenda kuingia mkataba na benki, kumbe benki pia ndyo imeichukua Ligi Kuu,”.
    “Kwa mfano mwaka 2013 tuliingia mkataba na Zantel tukiamini Vodacom kamaliza mkataba na haendelei, lakini siku tunasaini mkataba na Zantel, Vopdacom nao wakaenda kuongeza mkataba na TFF, matokeo yake sisi tulivuliwa jezi (zenye nembo ya Zantel) uwanjani wakati tunaingia kucheza,”.
    “Sasa mambo kama haya si vizuri kutokea, tunaomba TFF waseme mapema mdhamini wa Ligi Kuu msimu ujao ni nani, ili nasi tujjpange bila kuingilia maslahi yao,”amesema.
    Zamunda amesema kwa sasa ana uzoefu wa miaka minane ya kuendesha timu ya mpira wa miguu nchini Tanzania ambao anataka autumie kuhakikisha Lyon inafanya vizuri msimu ujao.
    African Lyon imekuwa ni timu yenye uzoefu wa kucheza na madaraja mawili, Ligi Kuu na Daraja la Kwanza tangu ipande kwa mara ya kwanza msimu wa 2009/2010.
    Ilipanda chini ya umiliki wa mfanyabiashara, Mohammed ‘Mo’ Dewji ambaye aliinunua kutoka kwa Jamal Kisongo na wafanyabiashara wa soko la Mbagala, ambaye naye akamuuzia Zamunda miaka miwili baadaye.
    Lyon ni kati ya timu sita zilizopanda Ligi Kuu msimu huu, nyingine ni KMC, JKT Tanzania za Dar es Salaam, Coastal Union ya Tanga, Biashara United ya Mara na Alliance Schools ya Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AFRICAN LYON WATAKA KUJUA MDHAMINI WA LIGI KUU MSIMU UJAO, WASEMA HAWATAKI KUVULIWA JEZI UWANJANI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top