• HABARI MPYA

  Monday, June 04, 2018

  SAMATTA AKUSANYA MAONI TAIFA STARS IFUZU AFCON…MMOJA ASEMA URAIA WA NCHI MBILI UTATUBEBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  NAHODHA wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta ameamua kukusanya maoni juu ya namna ya kufanya timu hiyo ifuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani nchini Cameroon.
  Samatta ameposti ujumbe; “Hivi ukipata nafasi ya kushauri chochote ambacho kinaweza kuifanya 'taifa stars'kupata tiketi ya afcon mwakani unadhan ungeshauri jambo gani? Nini kifanyike? Sina maana ushauri utafatwa ama la lakini tuongelee tu hili jambo hapa,”.
  Wadau mbalimbali wakiwemo Waandishi wa Habari na wachambuzi mashuhuri nao wameposti maoni yao, lakini mtu mmoja ametoa kichekesho kwa kusema wanawake 30 wa Tanzania wapelekwe Brazil, Ujerumani, Ufaransa, Argentina, Hispania na Afrika Magharibi wakabebeshwe mimba waje kuzaa watoto wenye vipaji vya kuinua soka la Tanzania.

  Mbwana Samatta (kulia) amekusanya maoni ya kuisaidia Taifa Stars ifuzu AFCON mwakani nchini Cameroon 

  Edo Kumwembe amesema kwa sasa Tanzania ina wachezaji wazuri kuliko wakati timu ilipokuwa chini ya kocha Mbrazil, Marco Maximo, lakini tatizo watu wanapenda zaidi Simba na Yanga na akaungwa mkono na Jeff Leah wote wakishauri hamasa irejeshwe.
  Harun Hamza akasema; “Kingine kaka na Serekali yetu inachangia kubomoa Taifa Stars, kwa nini isiruhusu wachezaji kuwa na uraia wa nchi mbili, asilimia kubwa ya nchi za wenzetu wanabebwa na uraia wa nchi mbili,”.
  Maoni ya Samatta yanakuja baada ya kushuhudiwa wiki ya mechi za kirafiki za kimataifa ikikatika bila Taifa Stars kucheza mechi – huku viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakiwa kimya.
  Inafahamika kocha Salum Mayanga amemaliza mkataba wake Machi na ilitarajiwa ama mzalendo huyo kuongezwa kandarasi, au kuajiriwa kocha mwingine kuendelea kuijenga Taifa Stars kwa mechi za kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).
  Baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka jana Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, Taifa Stars itasafiri kuwafuata Uganda Septemba 7, mwaka huu kabla ya kuwafuata Cape Verde Oktoba 10 kukamilisha mechi zake za mzunguko wa kwanza.
  Huu ulikuwa muda mzuri TFF iliyo chini ya Rais wake, Wallace Karia na Mtendaji Mkuu, Wilfred Kidau kuutumia kuiandaa timu kabla ya mechi na Uganda miezi mitatu tu ijayo, lakini hadi sasa hata kocha wa timu hajulikani.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SAMATTA AKUSANYA MAONI TAIFA STARS IFUZU AFCON…MMOJA ASEMA URAIA WA NCHI MBILI UTATUBEBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top