• HABARI MPYA

  Monday, June 11, 2018

  MWAKYEMBE AIPA MAMLAKA BMT KUSIMAMIA MCHEZO WA KUOGELEA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe ameipa mamlaka Baraza la Michezo la Tanzania (BMT) kusimamia shughuli za mchezo wa kuogelea wakati mchakato wa kuandaa uchaguzi mkuu wa chama hichon (TSA) ukiandaliwa.
  Waziri Mwakyembe alisema hayo jana katika kikao kilicho wakutanisha viongozi wa zamani walioenguliwa madarakani na wanachama wa chama hicho na Kamati ya Muda iliyomaliza muda wake wa miezi mitatu.
  Alisema kuwa TSA  imekuwa na mvutano wa uongozi kwa muda sasa na kuhatarisha maendeleo ya mchezo huo ambao umeifanya Tanzania kutambulika zaidi kwa nchi za Kanda ya Tatu (Cana zone three) ikiwa ni mabingwa mara mbili mfululizo.

  Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati) akisisitiza jambo wakati wa mkutano wa pamoja baina ya serikali na viongozi wa zamani wa Chama Cha Kuogelea Nchini (TSA) na kuamuru BMT kusimamia shughuli za mchezo huo wakati mchakato wa kuandaa uchaguzi mkuu ukiandaliwa. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara, Suzan Mlawi na Kaimu Katibu Mkuu wa BMT. Alex Nkeyenge.

  Mwakyembe alisema kuwa mbali ya BMT kusimamia mchezo huo kwa sasa, viongozi wa zamani chini ya mwenyekiti Alex Moshi na Katibu Mkuu, Ramadhani Namkoveka wanatakiwa kuwasilisha ripoti ya utendaji wao ikiwa pamoja na taarifa za fedha (mapatona matumizi) kwa Msajili wa Klabu na Vyama Vya Michezo.
  Alifafanua kuwa TSA ilitakiwa kufanya hivyo mwaka jana, lakini kutokana na hali ilivyokuwa, zoezi hilo lilisogezwa mbele mpaka Februari 28 mwaka huu, jambo ambalo halikufanyika.
  “Nawaagiza kuwasilisha taarifa za utendaji wenu haraka iwezekanavyo kwa Msajili, kinyume hayo, sheria itachukua mkondo wake, serikali ya Awamu ya Tano  haina mchezo mchezo kwa viongozi ambao hawawajibiki na tutafanya haya kwa kila chama cha michezo,” alisema Mwakyembe.
  Alisema kuwa  hata viongozi ambao walijihudhuru nafasi zao, wanatakiwa kuwasilisha taarifa zao mpaka pale walipoamua kuachana na uongozi.
  “Naipongeza Kamati ya Muda kwa kukamilisha kazi zao kwa muda wa miezi mitatu kama walivyopewa na BMT na kwa sasa suala la Katiba litajadiliwa na Kaimu Katibu Mkuu wa BMT, Msajili na viongozi wa zamani na Kamati hiyo siku ya Jumatano (June 13),” alisema.
  Kamati ya Muda iliyokuwa chini ya Mwenyekiti, Imani Dominick na Katibu wake, Inviolata Itatiro iliyomaliza muda wake Juni 9 mwaka huu. Wajumbe wengine wa kamati hiyo walikuwa, Alex Mwaipasi, Amina Mfaume na Anna Shanalingigwa.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MWAKYEMBE AIPA MAMLAKA BMT KUSIMAMIA MCHEZO WA KUOGELEA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top