• HABARI MPYA

  Monday, December 14, 2015

  YANGA SC KUMCHUKULIA HATUA ZA KINIDHAMU NIYONZIMA

  Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
  YANGA SC itamchukulia hatua za kinidhamu kiungo wake, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kwa kitendo cha kuchelewa kurejea katika timu baada ya majukumu ya kitaifa.
  Nahodha huyo wa Rwanda aliruhusiwa kwenda kuichezea timu yake ya taifa katika Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge nchini Ethiopia, lakini baada ya mashindano hajarejea Dar es Salaam.
  Katibu wa Yanga SC, Dk. Jonas Tiboroha amesema kwamba imekuwa kawaida kwa Niyonzima kila anapopewa ruhusa ya kurejea nchini kwao kuitumikia timu ya taifa, anachelewa kurudi.
  Haruna Niyonzima atachukuliwa hatua za kinidhamu baada ya kuchelewa kurudi Yanga SC

  Amesema tabia hiyo sugu ya Niyonzima imekuwa ikiiathiri timu kwa namna moja au nyingine, kwa sababu yeye ni mchezaji tegemeo katika timu.
  “Mfano hii mechi ya jana (Jumamosi dhidi ya Mgambo), tulitegemea yeye angekuwapo angeisaidia timu, hakuwepo matokeo yake tumetoa sare, sasa tunataka hadi mashabiki ambao wanampenda huyo mchezaji, wajue matatizo yake,”amesema Tiboroha.
  Katibu huyo amesema kwamba mara nyingi mchezaji huyo amekuwa akiondoka katika klabu kinyume cha taratibu, kwa sababu Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) huwa halitumi barua ya kumuombea ruhusa.
  “Hata safari hii, yeye aliondoka mapema mno akisema amepata msiba kwao na hakucheza mechi mbili za mwisho, lakini bado amechelewa kurudi. Mwenzake, Mugiraneza (Jean Baptiste) amerudi mapema Azam FC na amecheza dhidi ya Simba (Jumamosi), kwa nini yeye hajarudi?”amehoji Tiboroha.
  “Kinachosikitisha zaidi amezima simu zake zote kiasi kwamba sisi hatujui yuko wapi. Wakati alipokuwa Ethiopia, alikuwa anawasiliana na kocha (Hans van der Pluijm) na alijua umuhimu wa kuwahi, sasa kitendo hiki tukitafsiri vipi?”amehoji tena Tiboroha.
  Katibu huyo amesema kwamba Kamati ya Mashindano na Usajili chini ya Mwenyekiti wake, Isaac Chanji itakutana leo kujadili suala la mchezaji huyo na kuna uwezekano kabisa akachukuliwa hatua za kinidhamu, ili iwe fundisho kwa wengine wote.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: YANGA SC KUMCHUKULIA HATUA ZA KINIDHAMU NIYONZIMA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top