• HABARI MPYA

  Friday, June 09, 2023

  DUBE APIGA NNE AZAM FC YAITANDIKA POLISI TANZANIA 8-0


  TIMU ya Azam FC imehitimisha msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa ushindi wa mnono wa mabao 8-0 dhidi ya Polisi Tanzania leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Mabao ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji wake Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo manne dakika za nane, 15, 28 na 56, Kipre Junior dakika ya 20, Iddi Nado mawili dakika ya 40 na 75 na Yahya Zayd dakika ya 85.
  Azam FC inamaliza Ligi Kuu katika nafasi ya tatu kwa pointi zake 59, nne zaidi ya washindi wa nne Singida Big Stars na Namungo FC iliyomaliza na pointi 40 inakamilisha Tano Bora - wote wakiwa nyuma ya mabingwa, Yanga waliomaliza na pointi 78, tano zaidi ya washindi wa pili Simba SC.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, mabingwa Yanga wamemaliza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Mabao ya Yanga yamefungwa na mshambuliaji wake tegemeo, Fiston Kalala Mayele dakika ya 33 na Mkongo mwenzake, kiungo Yanick Bangala Litombo dakika ya 90 na ushei.
  Mshambuliaji wa Yanga Fiston Kalala Mayele amemaliza na mabao ya 17, sawa na kiungo Mrundi wa Simba, Saido Ntibanzokiza na wote wanakuwa wafungaji Bora.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Simba imeichapa Coastal Union 3-1 Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Simba yamefungwa na Ntibanzokiza mawili, dakika ya 14 na 73 na Nahodha, John Bocco dakika ya 56, wakati la Coastal Union limefungwa na Mbaraka Hamza kwa penalti dakika ya saba.
  Mechi nyingine, KMC imeichapa Mbeya City 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, Mtibwa Sugar imeichapa Geita Gold 1-0 Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro na Ihefu imeshinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya.
  Nayo Namungo FC imetoa sare ya 1-1 na Singida Big Stars Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na Dodoma Jiji imeshinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting mjini Morogoro.
  Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zimeshuka Daraja, wakati Mbeya City na KMC zitamenyana katika mechi mbili za nyumbani na ugenini kuwania kubaki Ligi Kuu.
  Timu itakayoshinda baada ya mechi hizo mbili kati ya Mbeya City na KMC itabaki Ligi Kuu na itakayofungwa itakwenda kumenyana na Mashujaa ya Kigoma kuwania kubaki Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: DUBE APIGA NNE AZAM FC YAITANDIKA POLISI TANZANIA 8-0 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top