• HABARI MPYA

    Wednesday, June 14, 2023

    SERIKALI KUJENGA KIWANJA KIPYA CHA MICHEZO JIJINI ARUSHA


    MKOA wa Arusha umepewa dhamana kubwa ya kitaifa ya kujengwa kiwanja kipya cha michezo na kufanya Tanzania kuwa na viwanja vitatu vinavyokidhi vigezo na mahitaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ili kuandaa mashindano ya AFCON 2027 katika ukanda wa Afrika Mashariki.
    Akikagua eneo kitakapojengwa kiwanja hicho kata ya Olmoti jijini Arusha la Juni 13, 2023, Mkuu wa mkoa huo Bw. John Mongela amesema mkoa umepokea mradi huo kwa mikono miwili na watatekeleza azma ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo makubwa barani Afrika.
    “Tunamshukuru Rais kwa moyo wake wa uzalendo wa kuwaletea watanzania maendeleo makubwa, Uwanja huu utabadilisha sana sura ya Mkoa wa Arusha na kuiweka kwenye ramani ya dunia, tutatekeleza maelekezo ya Wizara yetu ya michezo, maelekezo ya TFF, mwongozo wa Mhe. Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu na mamlaka zote. Sisi kama mkoa tutafanya linalowezekana jambo hili lifanikiwe” amesema Bw. Mongela.
    Ili kufikia azma ya Tanzania kuwa wenyeji wa AFCON 2027 kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda, tayari Kiwanja cha Benjamin Mkapa cha Dar es salaam kimeanza kufanyiwa ukarabati mkubwa pamoja na Kiwanja cha Amani Zanzibar hatua itakayofanya Tanzania kuwa na viwanja vitatu vinavyokidhi ubora kulingana na Sharia na Kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) pamoja na mashindano mengine duniani.
    Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amesema lengo la ziara hiyo ni kukagua eneo kitakapojengwa kiwanja cha kisasa cha michezo katika jiji la Arusha ambayo ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.
    “Huu ni ukaguzi wa awali wa eneo utakapojengwa uwanja wa michezo hapa Arusha,  Sisi Wizara tunawaahidi wakazi wa mkoa wa Arusha pamoja na Watanzania kwa ujumla kuwa tutajenga kiwanja cha kisasa chenye uwezo wa kuchukua watu 30,000,000 ambacho kina uwezo wa kuchezwa mechi za CAF na mechi ambazo zinatambuliwa na FIFA” amesema Bw. Yakubu.
    Aidha, ziara hiyo imeshirikisha Uongozi wa mkoa wa Arusha, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SERIKALI KUJENGA KIWANJA KIPYA CHA MICHEZO JIJINI ARUSHA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top