KLABU ya Simba SC imeachana na kiungo wake mkongwe na kipenzi cha mashabiki, Jonás Gerard Mkude aliyedumu kikosini kwa miaka 13 tangu apandishwe kutoka timu ya vijana.
“Uongozi wa klabu unatoa shukrani za dhati kwa mchango mkubwa aliotoa kwenye timu yetu kiungo mkabaji, Jonas Mkude katika muda wote wa miaka 13 aliyodumu nasi,” imesema taarifa ya Simba jioni hii na kuongeza.
“Tunamtakia kila la kheri kwenye changamoto mpya ya maisha ya soka nje ya Simba,”.
Jonás Mkude anakuwa mchezaji wa saba kuachwa Simba baada ya kipa Beno Kakolanya, beki Muivory Coast, Mohamed Ouattara, na viungo Erasto Nyoni, Wanigeria, Nelson Okwa, Víctor Akpan na Mghana, Augustine Okrah.
Simba pia imeachana na makocha wake wawili wa Fiziki, Kelvin Mandla Ndlomo na Fareed Cassiem, wote raia wa Afrika Kusini na kocha wa makipa, Mmorocco, Zakaria Chlouha na kocha wake wa timu yake ya wanawake, Mganda Charles Lukula.
0 comments:
Post a Comment