• HABARI MPYA

  Friday, June 09, 2023

  SIMBA SC YAMALIZA NA USHINDI WA 3-1 DHIDI YA COASTAL


  TIMU ya Simba imekamilsha msimu wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kwa ushndi wa mabao 3-1 dhidi ya Coastal Union leo Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam.
  Mabao ya Simba yamefungwa na Ntibanzokiza mawili, dakika ya 14 na 73 na Nahodha, John Bocco dakika ya 56, wakati la Coastal Union limefungwa na Mbaraka Hamza kwa penalti dakika ya saba.
  Simba SC inamaliza Ligi na pointi 73, ikizidiwa tano na mabingwa, Yanga SC, wakati Azam FC imemaliza na pointi 59 nafasi ya tatu, Singida Big Stars pointi 55 nafasi ya nne na Namungo FC pointi 40 nafasi ta tano.
  Mechi nyingine za Ligi Kuu leo,Yanga imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine Jijini Mbeya.
  Mabao ya Yanga yamefungwa na mshambuliaji wake tegemeo, Fiston Kalala Mayele dakika ya 33 na Mkongo mwenzake, kiungo Yanick Bangala Litombo dakika ya 90 na ushei.
  Mshambuliaji wa Yanga Fiston Kalala Mayele amemaliza na mabao ya 17, sawa na kiungo Mrundi wa Simba, Saido Ntibanzokiza na wote wanakuwa wafungaji Bora.
  Nayo Azam FC imeitandika Polisi Tanzania Mabao 8-0 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
  Mabao ya Azam FC yamefungwa na mshambuliaji wake Mzimbabwe, Prince Dube Mpumelelo manne na mengine Kipre Junior, Iddi Nado mawili na Yahya Zayd.
  Mechi nyingine, KMC imeichapa Mbeya City 1-0 Uwanja wa Nelson Mandela, Sumbawanga mkoani Rukwa, Mtibwa Sugar imeichapa Geita Gold 1-0 Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Ihefu imeshinda 2-0 dhidi ya Kagera Sugar Uwanja wa Highland Estate, Mbarali mkoani Mbeya, Namungo FC imetoa sare ya 1-1 na Singida Big Stars Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa mkoani Lindi na Dodoma Jiji imeshinda 1-0 dhidi ya Ruvu Shooting mjini Morogoro.
  Ruvu Shooting na Polisi Tanzania zimeshuka Daraja, wakati Mbeya City na KMC zitamenyana katika mechi mbili za nyumbani na ugenini kuwania kubaki Ligi Kuu.
  Timu itakayoshinda baada ya mechi hizo mbili kati ya Mbeya City na KMC itabaki Ligi Kuu na itakayofungwa itakwenda kumenyana na Mashujaa ya Kigoma kuwania kubaki Ligi Kuu.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA SC YAMALIZA NA USHINDI WA 3-1 DHIDI YA COASTAL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top