• HABARI MPYA

    Thursday, November 02, 2017

    ERASTO NYONI MCHEZAJI BORA WA MWEZI SIMBA SC

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    BEKI wa pembeni wa Simba, Erasto Edward Nyoni ameshinda tuzo ya Mchezaji Bora wa mwezi Oktoba wa klabu hiyo.
    Nyoni, mwenye umri wa miaka 29 sasa ameshinda tuzo hiyo baada ya kazi nzuri katika mwezi Oktoba akiisaidia klabu yake kuongoza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
    Pamoja na umri wake mkubwa, lakini Nyoni amekuwa akifanya kazi nzuri, kuliko wachezaji vijana wadogo akilinda vizuri na kusaidia mashambulizi kwa kupanda na kupiga krosi nzuri kusaidia upatikanaji wa mabao. 
    Kwa ushindi huo, pamoja na kujiweka kwenye nafasi ya kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Msimu wa klabu, Nyoni pia atazawadiwa kitita cha Sh. 500,000. 
    Pamoja na kuwa tegemeo la klabu yake mpya, Simba aliyojiunga nayo Julai akitokea Azam FC, Nyoni ni mchezaji tegemeo wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
    Erasto Nyoni alicheza kwa dakika zote 90 katika mchezo dhidi ya mahasimu, Yanga Jumamosi
    Erasto ni mchezaji pekee ambaye alikuwepo timu ya taifa kanzia wakati wa Mbrazil, Marcio Maximo mwaka 2006 na ameendelea kuitwa na kila kocha aliyefuatia kupewa jukumu la kuifundisha timu hiyo kuanzia Wadenmark Jan Borge Poulsen, Kim Poulsen, Mholanzi, Mart Nooij na wazalendo Mkwasa na huyu wa sasa, Salum Mayanga.
    Pamoja na kucheza nafasi za ulinzi, lakini Nyoni ameifungia Stars mabao manne ya kukumbukwa, likiwemo bao pekee katika ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji Burkina Faso, Juni 16, mwaka 2007 mjini Ouagadougou katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2010.
    Na hilo ndilo lilikuwa bao lake la kwanza Taifa Sars kabla ya kufunga tena Juni 10, mwaka 2012 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao la ushindi, Tanzania ikiilaza 2-1 Gambia katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.
    Akafunga bao la kwanza katika sare ya 3-3 na wenyeji Botswana Uwanja wa Molepolole mjini Molepolole, Agosti 15, 2012 kwenye mchezo wa kirafiki, kabla ya Julai 5, mwaka huu kufunga bao la kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la COSAFA Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikifungwa 4-2 na Zambia waliotoka nyuma kwa 1-0.
    Nyoni alijiunga na Azam FC mwaka 2010 akitokea Vital’O ya Burundi iliyomchukua AFC ya Arusha alikocheza kidogo tu akitokea kituo cha Rollingston cha mjini humo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ERASTO NYONI MCHEZAJI BORA WA MWEZI SIMBA SC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top