• HABARI MPYA

  Jumapili, Novemba 26, 2017

  YANGA YAMSAJILI BEKI MKONGO, BOSSOU NDIYO BASI TENA

  Na Salma Suleiman, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Yanga jana imemsainisha mkataba wa miaka miwili, beki wa kati, Mkongo Fiston 'Festo' Kayembe Kanku ambaye alikuwa kwenye majaribio katika timu hiyo kwa muda mrefu.
  Usajili huo unakuja siku moja baada ya safu ya ulinzi ya Yanga kuruhusu bao la tano katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana wakilazimishwa sare ya 1-1 na Tanzania Prisons Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Usajili wa Kayembe unazima kabisa uwezekano wa beki Mtogo, Vincent Bossou kurejeshwa Jangwani, licha ya kupigiwa debe na wadau mbalimbali wa klabu hiyo, arejeshwe kikosini.
  Bossou alimaliza mkataba wake msimu uliopita baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka miwili alitarajiwa kuendelea kutokana na kufanya vizuri, lakini klabu haikumpa mkataba mpya baada ya mazungumzo ya muda mrefu.
  IlifikiRIwa hali mbaya ya kiuchumi ilisababisha Yanga kumwaka kumpa mkataba mpya Bossou, lakini kitendo cha klabu kumsajili Kayembe anayetokea Balende FC ya kwao, Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo (DRC) kinaashiria imeamua kuachana na Mtogo huyo kwa vyovyote.
  Licha ya kucheza pungufu ya mchezaji mmoja, Tanzania Prisons imefanikiwa kupata sare ya ugenini ya kufungana 1-1 na wenyeji, Yanga SC katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Sare hiyo inaifanya Yanga SC iendelee kukamata nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu, nyuma ya Simba na Azam ambazo pia zina mechi moja moja mkononi. 
  Katika mchezo huo uliochezeshwa na Shomary Lawi wa Kigoma aliyesaidiwa na Abdallah Rashid wa Pwani na Sylvester Mwanga wa Kilimanjaro, hadi mapumziko tayari timu hizo zilikuwa zimekwishafungana mabao hayo.
  Prisons walitangulia kwa  bao la Eliuter Mpepo dakika ya tisa akitumia makosa ya mabeki wa kati wa Yanga, Andrew Vincent ‘Dante’ na Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ waliochanganyana na kipa wao, Mcameroon, Youth Rostande na kushindwa kuokoa.
  Prisons walipata pigo dakika ya 36 baada ya mchezaji wake, Lambert Sibiyanka kutolewa kwa kadinyekundu na refa Lawi kufuatia kumpiga kiwiko beki wa Yanga, Juma Abdul.
  Yanga walitumia mwanya huo kuongeza mashambulizi kusaka bao la kusawazisha na wakafanikiwa kupata bao dakika ya 41, lililofungwa na kiungo Raphael Daudi aliyemalizia krosi ya mshambuliaji Ibrahim Ajib.
  Kwa sare hiyo, Yanga inafikisha pointi 21 baada ya kucheza mechi 11, ikizidiwa pointi mbili mbili na zote, Simba na Azam. Simba watawakaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Uhuru kesho na Azam watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Chamazi Jumatatu.   
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: YANGA YAMSAJILI BEKI MKONGO, BOSSOU NDIYO BASI TENA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top