• HABARI MPYA

  Sunday, November 26, 2017

  AZAM ILIHITAJI KUJARIBU NCHI NYINGINE BAADA YA WAGHANA KUCHEMSHA MFULULIZO

  WIKI hii Azam FC imemsajili mshambuliaji mpya Mghana, Bernard Arthur kutoka klabu ya Liberty Professional ya Ghana.
  Arthur amesaini mkataba wa miaka miwili kujiaunga na matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, na zoezi zima limefanikishwa na Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohammed, aliyekuwepo nchini Ghana kukamilisha usajili wake.
  Azam wamesema usajili wa Arthur mwenye umri wa miaka 20, ni sehemu ya mapendekezo ya benchi la ufundi la timu hiyo kwenye usajili huu wa dirisha dogo, anayekuja kuziba pengo la straika mwingine, Yahaya Mohammed, aliyeondoka kwa makubaliano maalumu ya pande mbili wiki chache zilizopita.
  Mshambuliaji huyo wa zamani wa timu ya WAFA (Ghana) na Asec Mimosa ya Ivory Coast, anaungana na washambuliaji wengine wa timu hiyo katika kukiongezea makali kikosi hicho, ambao ni Mbaraka Yusuph, Wazir Junior, Yahya Zayd, Shaaban Idd pamoja na wale waliopandishwa kutoka Azam B, Paul Peter na Andrea Simchimba.
  Liberty Professional ni moja ya kitovu kikubwa cha kutoa mastaa wa baadaye nchini Ghana, wachezaji waliotesa barani Ulaya waliowahi kupiatia hapo ni nyota wa zamani wa Chelsea, Michael Essien, Sulley Muntari (Pescara, Italia) na Asamoah Gyan (Kayserispor, Uturuki).
  Azam FC ina matumaini makubwa kuwa usajili wa nyota huyo, utaweza kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji na kutatua tatizo la ukosefu wa mabao linaloonekana, hii ikitarajia kuendeleza mbio za kuwania taji la Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania walizozianza vema hadi sasa.
  Aidha uongozi kwa ujumla na Bodi ya Wakurugenzi ya Azam FC, unaendelea kutoa pongezi kwa mashabiki wa timu kwa moyo wanaoendelea nao wa kuisapoti timu hiyo, kwa hakika kila mmoja amejionea namna nguvu na umoja wao wa kuishangilia timu unavyozidi kuwapa hamasa wachezaji na kupata matokeo bora kwenye kila mchezo.
  Arthur aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya vijana ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (Ghana U-20), ni mmoja wa washambuliaji bora kwa sasa katika Ligi Kuu nchini Ghana (GPL), msimu huu akifunga jumla ya mabao 11, tisa akifunga ndani ya ligi hiyo na mawili (Kombe la FA).
  Moja ya sifa zake kubwa ni uwezo wa kumiliki mpira na kuwatoka mabeki wa timu pinzani kwa spidi, kukaa na mipira na kusambaza kwa wachezaji wenzake, kutumia vizuri miguu yote miwili, uwezo wa kupiga mashuti kwenye eneo lolote la ushambuliaji pamoja na kusaidia ukabaji pale timu pinzani inapokuwa ikishambulia.
  Arthur alianzia soka lake katika timu ya Mighty Cosmos kwenye eneo alilozaliwa na kukulia la Dansoman nchini Ghana, akiwa kijana mdogo mwaka 2005-2010.
  Cosmos aliyoanzia soka lake Arthur, pia wamewahi kucheza nyota wengi wa soka la Ghana wakiwamo nahodha wa zamani na timu ya Taifa ‘Black Star’, Stephen Appiah na Michael Essien.
  Mbali na kucheza Liberty, mshambuliaji huyo pia amewa kucheza kwa mabingwa wa msimu uliopita nchini Ghana, WAFA huku pia akiwahi kutolewa kwa mkopo kujiunga kwa vigogo wa Ivory Coast, Asec Mimosa.
  Nyota huyo anayejaribu kufuata nyayo za mshambuliaji nyota wa Ghana, Asamoah Gyan, anakwenda kuwa Mghana wa tano kwenye kikosi cha Azam wengine, kipa Razack Abalora, mabeki Daniel Amoah, Yakubu Mohammed na kiungo Enock Atta - Agyei ambao wanaungana na beki Mzimbabwe, Bruce Kangwa na kiungo Mcameroon, Stephanne Mpondo Kingue.
  Kabla ya kuondoka kwa Yahya, Azam FC ilimtema mshambuliaji mwingine Mghana,  Samuel Afful baada ya nusu msimu tu wa kufana kazi Chamazi.
  Afful na Yahya waliletwa kwa pamoja na wakala wao, Kingsley Atakorah, ambaye pia ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Adom Wonders Academy ya nchini Ghana – lakini aliondoka kimya kimya.
  Wakati Afful iliyeelezwa ana umri wa miaka 20, alisaini mkataba wa miaka mitatu, Yahya alisaini miaka miwili.
  Afful alisajiliwa akiwa timu za vijana za Ghana chini ya umri wa miaka 20 na 23 na akitokea klabu ya Sekondi Hasaacan ya Ghana, ambayo alikuwa kinara wa mabao.
  Rekodi zake nyingine ni kuifungia bao muhimu timu ya Taifa ya Ghana chini ya umri wa miaka 20 (U-20) mwaka juzi dhidi ya Zambia kwenye ushindi wa mabao 2-1, lililoipa nafasi ya kushiriki fainali za Kombe la Dunia nchini New Zealand, baada ya kutinga nusu fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana (U-20) zilizofanyika Senegal mwaka jana.
  Yahya aliyekuwa ana umri wa miaka 28 wakati anasajiliwa Novemba mwaka jana, alikuwa anatokea Aduana Stars ambako alikuwa mfungaji bora namba mbili wa Ligi Kuu ya Ghana msimu uliotangulia akifunga mabao 15, pungufu ya mabao mawili ya kinara Latif Blessing wa Liberty Proffessional aliyemaliza na mabao 17.
  Unaweza kuona wachezaji walioondoka walisajiliwa wakiwa wana wasifu mzuri kuliko Arthur anayeingia sasa.
  Na kihistoria wachezaji wa kwanza kabisa wa Ghana kujiunga na Azam FC walisajiliwa mwaka 2011, beki wa kushoto Nafiu Awudu na mshambuliaji Wahab Yahya waliotokea klabu ya King Faisal ya kwao.
  Lakini wachezaji hao hawakufanya vizuri Azam FC na ndani ya msimu mmoja wakatemwa. Hata wachezaji waliopo sasa Azam FC, wanafanya vizuri katika kiwango cha kawaida, bado hawajaonyesha uwezo wa kustaajabisha kujitofautisha wazawa wanaosajiliwa kwa gharama nafuu.
  Namaanisha Azam FC ilihitaji kujaribu sehemu nyingine baada ya kuachana na washambuliaji wawili mfululizo kutoka Ghana, Yahya na Afful – lakini katika mastaajabu ya wengi imerudi tena Ghana. 
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM ILIHITAJI KUJARIBU NCHI NYINGINE BAADA YA WAGHANA KUCHEMSHA MFULULIZO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top