• HABARI MPYA

  Alhamisi, Novemba 23, 2017

  MSUVA AWATUNGUA MABINGWA WA AFRIKA…LAKINI DIFAA YAFA 2-1 KWA WYDAD LIGI YA MOROCCO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva jana ameifungia timu yake, Difaa Hassan El –Jadida bao la kupangusia machozi ikichapwa 2-1 na mabingwa wa Afrika, Wydad Casablanca katika mchezo wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Prince Moulay Abdallah mjini Rabat, wenyeji walitangulia kwa mabao mawili kipindi cha kwanza, kabla ya Msuva kuifungia bao hilo moja Difaa Hassan El -Jadida kipindi cha pili. 
  Pamoja na kufungwa, Difaa Hassan El –Jadida walicheza vizuri na kutengeneza nafasi nzuri za mabao, lakini wakashindwa kuzitumia.
  Winga Simon Msuva akipambana kupita katikati ya mabeki wa Wydad Casablanca usiku wa jana
  Simon Msuva (katikati) mstari wa mbele kwenye kikosi cha kwanza cha Difaa Hassan El- Jadida jana

  Kipigo cha jana kinaongeza machungu kwa Difaa Hassan El –Jadida, kwani mchezo uliopita, Novemba 18 walitolewa katika Nusu Fainali ya Kombe la Ligi  na Raja Casablanca kwa penalty 3-1 baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika ya 120. 
  Difaa Hassan El-Jadida watateremka tena uwanjani Jumapili kumenyana na Racing de Casablanca katika mchezo mwingine wa Botola, Uwanja wa Pere-Jego mjini Casablanca.
  Ikumbukwe, Wydad ndiyo wafalme wapya wa soka barani, baada ya Novemba 5, mwaka huu kuichapa 1-0 Al Ahly ya Misri katika mchezo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Uwanja wa Mohammed V mjini Casablanca, bao pekee la Walid El Karty dakika ya 69.
  Wydad walibeba taji hilo la Afrika kwa ushindi wa jumla wa 2-1 baada ya kulazimisha sare ya 1-1 mjini Alexandria wiki iliyotangulia katika mchezo wa kwanza wa fainali.
  Kikosi cha Difaa Hassan El-Jadida jana kilikuwa; Yahia El Filali, Youssef Aguerdoum, Marouane El Hadhoudi, Fabrice Ngah, Mohamed Hamami/Youness Hawassi, Mohammed Ali Bemammer, Mario Mandrault/Hamid Ahadad, Ayoub Nanah, Bilal El Magri/Tarik Astati, Simon Msuva na Adnane El Ouardy.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MSUVA AWATUNGUA MABINGWA WA AFRIKA…LAKINI DIFAA YAFA 2-1 KWA WYDAD LIGI YA MOROCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top