• HABARI MPYA

  Jumatatu, Novemba 27, 2017

  MTIBWA SUGAR: TUMEKUJA DAR KIKAMILIFU KUIVAA AZAM LEO

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  MTIBWA Sugar ya Morogoro imesema kwamba imekuja Dar es Salaam kikamilifu kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC leo Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
  Meneja wa Mtibwa Sugar, mabingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, 1999 na 2000, Sidy Ibrahim amesema kwamba wako tayari kwa mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkali timu hizo zinapokutana. 
  “Tunatarajia mchezo utakuwa mgumu kwa sababu ndiyo kawaida kila tunapokutana na Azam mchezo huwa mgumu. Lakini sisi tumejiandaa vizuri na tumekuja hapa kikamilifu kwa ajili ya mchezo wenyewe,”amesema Meneja huyo.
  Meneja wa Mtibwa Sugar, Sidy Ibrahim (mwenye kofia) amesema wako tayari kwa mchezo na Azam leo 

  Mtibwa Sugar iliyo chini ya kocha wake, Zuberi Katwila, ambaye ni mchezaji wake wa zamani, inatarajiwa kukutana na upinzani mkali mbele ya mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 2013, Azam FC.
  Azam FC wanahitaji ushindi katika mchezo wa leo ili kupanda kileleni mwa Ligi Kuu, kufuatia vigogo Simba na Yanga wote kulazimishwa sare za 1-1 mwishoni mwa wiki na Tanzania Prisons ya Mbeya na Lipuli ya Iringa.
  Baada ya sare hizo na timu za Nyanda za Juu Kusini, Simba wanaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 23, wakati Yanga wana pointi 21 katika nafasi ya tatu baada ya mechi 11 – Azam FC ikiwa na pointi 22 katika nafasi ya pili. 
  Kikosi cha Mtibwa Sugar kilichokuja Dar es Salaa kwa ajlia ya mchezo huo kinaundwa na makipa; Benedictor Tinocco na Abuutwalib Msheri, mabeki; Rodgers Gabriel ‘Jigwa’, Issa Rashid ‘Baba Ubaya’, Hassan Mganga ‘Timbe’, Hussein Idd, Dickson Daudi, Cassian Ponera na Hassan Isihaka
  Viungo’ Shaaban Nditi, Ally Makarani, Mohamed Issa, Hassan Dilunga, Saleh Khamis, Ismail Aidan, Haruna Chanongo, Salum Kihimbwa na washambuliaji ni Stamil Mbonde, Kelvin Sabato, Hussein Javu na Riphat Khamis.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 maoni:

  Item Reviewed: MTIBWA SUGAR: TUMEKUJA DAR KIKAMILIFU KUIVAA AZAM LEO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
  Scroll to Top